Iran: Korea Kusini lazima itulipe deni letu
(last modified Fri, 07 Jan 2022 03:34:28 GMT )
Jan 07, 2022 03:34 UTC
  • Iran: Korea Kusini lazima itulipe deni letu

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa na kiongozi wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya Vienna amesema Korea Kusini haina chaguo jingine isipokuwa kutekeleza wajibu wake na kuilipa Jamhuri ya Kiislamu deni lake.

Ali Baqeri Kani alitoa mwito huo jana Alkhamisi katika mazungumzo yake na Choi Jong Kun, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini pambizoni mwa mkutano wa Vienna na kuongeza kuwa, serikali ya Seoul inapaswa kulilipa taifa la Iran deni lake, bila kujali matokeo ya mazungumzo hayo ya kuindolea Iran vikwazo vya kidhalimu.

Baqeri Kani ameeleza bayana kuwa, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani havipaswi kutumiwa na Korea Kusini kama hoja ya kuendelea kuzuilia fedha za Iran.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa ameitaka Seoul ichukue hatua za makusudi za kuipa Iran fedha zake, akisisitiza kuwa kuendelea kuzuia mali hizo za Tehran kutatia doa katika ukurasa wa historia ya uhusiano wa nchi mbili hizi.

Mkutano wa Vienna

Hata hivyo Ali Baqeri Kani katika hatua nyingine amesisitiza kuwa zimepigwa hatua nzuri katika suala la uondoaji vikwazo, kwenye duru ya nane ya mazungumzo yanayoendelea huko Vienna, Austria.

Kwa upande wake, Choi Jong Kun, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini amesema uhusiano wa Seoul na Tehran una umuhimu mkubwa, na kwamba serikali yake inafanya jitihada za kuachia fedha za Jamhuri ya Kiislamu.