Iran yapinga kutumiwa haki za binadamu kama chombo dhidi ya nchi zingine
Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Iran amekutana na mabalozi wa Russia na China nchini Iran ambapo wametangaza kwa pamoja kupinga kutumiwa vibaya kadhia ya haki za binadamu kama chombo cha kuyashinikiza mataifa mengine.
Levan Dzhagaryan, Balozi wa Russia, na Chang Hua, Balozi wa China nchini Iran wamekutana kwa nyakati tafauti na Kazem Gharibabadi Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Iran ambaye pia ni mkuu wa masuala ya kimataifa katika Idara ya Mahakama ya Iran. Katika mikutano hiyo, Gharibabadi ameashiria ushirikiano wa kistratijia baina ya Iran, Russia na China huku akisisitiza haja ya kustawisha ushirikiano katika nyanja za sheria, uadilifu na haki za binadamu.
Balozi wa Russia ameunga mkono pendekezo hilo na kusisitiza kuhusu, kuendelea kupinga maazimio ya haki za binadamu dhidi ya Iran na hatua zozote dhidi ya Iran katika uga huo.
Kwa upande wake balozi wa China amesema matukio ya kisiasa na kimataifa hayawezi kubadili irada ya nchi yake katika kushirikiana na Iran. Amesema China inalaani vikali hatua ya madola ya Magharibi kuingilia mambo ya ndani ya Iran kwa visingizio vya haki za binadamu.
Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani ni wakiukaji wakubwa zaidi wa haki za binadamu na zimekuwa zikitumia kadhia ya haki za binadamu kuhadaa umma katika nchi zao na kote duniani. Aidha madola hayo ya Magharibi yamekuwa yakitumia vibaya kadhia ya haki za binadamu kuzishinikiza nchi ambazo zinapinga ubeberu wa Kimagharibi.
Hivi sasa nchi tatu muhimu duniani, yaani Iran, Russia na China zimekuwa zikilengwa zaidi kwa tuhuma hizo zisizo na msingi za madola ya Magharibi zinazodai kuwa watetezi wa haki za binadamu na uhuru wa maoni. Madola hayo ya Magharibi yakiongozwa na Marekani hujidai kuwa polisi wa dunia na kwa msingi huo hutoa ripoti za kila mwaka za hali ya haki za binadamu katika nchi zingine hususan nchi ambazo zinatazamwa kama maadui wa Marekani ambapo hulengwa kwa propaganda za kisiasa na vyombo vya habari.
Hii ni katika hali ambayo, hivi sasa Marekani ni mkiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani. Kwa mujibu wa Andranik Migranyan, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Russia, Marekani ni mkiukaji mkubwa wa haki za binadamu duniani na imezishinda nchi nyingi katika uga huo.
Swali ambalo linaibuka hapa ni hili kuwa je, ni kwa nini Marekani inajiona kuwa inastahili kutoa ripoti na maoni kuhusu haki za binadamu katika nchi zingine duniani?
Pamoja na kuwa Marekani imekuwa ikitoa madai kuwa inazingatia haki za binadamu na uhuru wa mtu binafsi na jamii nchini humo, lakini madai hayo hayana ukweli wowote kwani utendaji wa serikali ya Marekani unaonesyha namna haki za binadamu zinavyokiukwa katika nchi hiyo. Walimwengu katika miaka ya hivi karibuni wameshuhudia namna ambavyo utawala wa Marekani unawabagua na kuwakandamiza Wamarekani asili na pia hakuna asiyejua kuwa Wamarekani wenye asili ya Afrika wamekuwa wakibaguliwa na kukandamizawa kinyama hasa mikononi mwa polisi nchini Marekani. Hali kadhalika polisi ya Marekani imekuwa na muamala mbovu sana na wahamiaji wa kigeni wakiwemo watoto wadogo ambao wanashikiliwa katika magereza ya kuogofya. Hali kadhalika mfumo wa utawala wa Marekani unawabagua na kuwakandamiza Waislamu kwa sababu tu ya itikadi yao.
Nukta nyingine ni kuwa, nchi za Magharibi zinapuuza ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi ambazo ni washirika wao. Mfano wa wazi wa hili ni kadhia ya vita vya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya watu wasio na hatia wa Yemen kwa muda wa miaka saba sasa. Muungano huo vamizi wa Saudia umeua makumi ya maelefu ya raia, wengi wakiwa ni wanawake na watoto sambamba na kuizingira nchi hiyo na hivyo kuzuia misaada ya kibinadamu na ya dharura kama vile dawa na chakula kuwafikia Wayemen. Pamoja na kuwepo ukiukaji huo mkubwa wa haki za binadamu, Rais Joe Biden wa Marekani ambaye katika kampeni zake aliahidi kuishurutisha Saudia iheshimu haki za binadamu sasa amesahau ahadi hizo na hata anaendelea kuiuzua Saudia silaha angamizi zinazotumika kuwaua raia wasio na hatia wa Yemen.
Katika upande mwingine, Biden anatumia visingizio mbali mbali kuzishinikiza Iran, Russia na China na kudai kuwa nchi hizi zinakiuka haki za binadamu na tuhuma kama hizo zinatolewa katika fremu ya vita vya kipropangadna dhidi ya nchi hizo tatu.