Kuuawa Luteni Jenerali Soleimani ni pigo kubwa kwa mapambano dhidi ya ugaidi
Mwakilishi wa Iran katika kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la umoja wa Mataifa amesema, kitendo cha serikali ya Marekani cha kumuua shahidi Luteni Jenerali Qasem Soleimani kilisababisha pigo kubwa kwa mapambano dhidi ya ugaidi wa eneo.
Kikao cha 49 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kilifanyika jana mjini Geneva kwa kusomwa taarifa ya asasi za kiraia za nchi mbalimbali duniani.
Kikao cha kila mwaka cha Baraza la Haki za Binadamu la UN kinafanyika mjini Geneva, ambapo kwa upande wa Iran wawakilishi wa asasi za kiraia wamehudhuria kikao hicho na kuhutubia kuhusu mapambano ya Iran dhidi ya ugaidi kwa upande wa ndani na katika mazingira ya kikanda, jinsi ugaidi wa kiserikali na usio wa kiserikali ulivyoigharimu Jamhuri ya Kiislamu na pia kuhusu namna baadhi ya nchi zinavyounga mkono ugaidi ndani ya Iran.
Asasi ya kiraia ya Iran iliyoshiriki katika mkutano huo kwa anuani ya "Asasi Iliyoathiriwa na Madhara ya Kijamii" imeeleza katika taarifa yake kuhusu mapambano ya Iran dhidi ya ugaidi na watu wake waliouawa shahidi katika njia hiyo na ikalilalamikia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa kutofanya chochote kuhusiana na ugaidi wa kiserikali wa Marekani.
Maryam Yousuf Safari, mjumbe wa Asasi Iliyoathiriwa na Madhara ya Kijamii ambaye ndiye aliyesoma taarifa ya asasi hiyo amesema, janga la ugaidi na misimamo ya kufurutu mpaka linajionyesha kwa sura mpya kila uchao.
Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema, kuuliwa Luteni Jenerali Qasem Soleimani akiwa katika ziara rasmi nchini Iraq lilikuwa pigo kwa misingi na taratibu zote za sheria za kimataifa na kusababisha athari haribifu kwa amani ya eneo; na kama hapo kabla ilikuwepo shaka yoyote juu ya Marekani kwamba ni muungaji mkono wa ugaidi, mauaji hayo yalimfanya kila mtu abainikiwe wazi zaidi na lengo la Marekani la kulitumbukiza eneo kwenye machafuko, kuvuurga amani na usalama na kuzichinja haki za binadamu.
Luteni Jenerali Qasem Soleimani, kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambaye Januari 3, 2020 alikuwa ameelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, aliuawa shahidi yeye na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa jeshi la kujitolea la wananchi wa Iraq la Al Hashdu-Sha'abi pamoja na wanamuqawama wengine wanane usiku wa manane wa kuamkia siku hiyo katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad nchini Iraq.../