Iran iko tayari kuisaidia Qatar kuandaa Kombe la Dunia kwa mafanikio
Katika mazungumzo ya simu na Amir wa Qatar, Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu Iran amesisitiza utayarifu wa Iran katika kuisaidia nchi hiyo kuandaa kwa mafanikio Kombe la Dunia.
Kwa mujibu wa IRNA, Seyyed Ebrahim Raisi Jumapili usiku akijibu simu kutoka kwa Sheikh Hamad bin Tamim Al Thani Emir wa Qatar, amemtumia pongezi kwa mnasaba wa kuwadia mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuelezea kuridhishwa na kufanyika michezo ya Kombe la Dunia la FIFA nchini Qatar. Ameitakia mafanikio nchi hiyo katika kuandaa hafla hiyo muhimu ya kimichezo na kusema: 'Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutoa msaada na usaidizi unaohitajika ili kufanikisha michezo ya Kombe la Dunia katika Kisiwa cha Kish na visiwa vingine vilivyo karibu na Qatar, na sisi tumeridhishwa na mipango ambayo imefanywa katika uwanja hup.'
Akizungumzia uwezekano mkubwa wa kuongezwa kiwango cha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili, Raisi ameongeza kuwa: 'Tehran na Doha zinaweza kuchukua hatua madhubuti kuelekea maslahi ya pamoja na kuleta utulivu na usalama katika eneo kwa maslahi ya mataifa ya eneo."

Akiashiria safari inayotazamiwa kufanywa hivi karibuni na Amir wa Qatar mjini Tehran, Rais wa Iran amebainisha: "Katika ziara hii, maamuzi mahimu yatatolewa kwa ajili ya kustawishwa zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya nchi mbili katika nyuga mbalimbali."
Ayatullah Raisi huku akieleza kuwa leo irada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Qatar imejikita katika kustawisha zaidi uhusiano wa pande mbili amesema: 'Tehran inakaribisha kustawishwa uhusiano na Doha katika nyanja mbalimbali na kuchukuliwa hatua muhimu za kuboresha zaidi uhusiano kati ya nchi hizi mbili.'
Amir wa Qatar pia amesisitiza katika mazungumzo hayo ya simu kwamba nchi yake imejitolea kikamilifu kuendeleza uhusiano na Tehran baada ya kufanyika vikao na mazungumzo marefu kati ya nchi hizi mbili huko Doha.
"Sheikh Hamad bin Tamim Al Thani" ameeleza kufurahishwa kwake na ushiriki wa timu ya taifa ya kandanda ya Iran katika Kombe la Dunia na kusema: "Tutawakaribisha vyema ndugu zetu katika mashindano haya."
Droo ya Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar ilifanyika Ijumaa usiku katika mji mkuu wa Doha. Kwa mujibu wa droo hiyo, timu ya taifa ya kandanda ya Iran itachuana katika Kundi B na Uingereza, Marekani na mshindi wa mchujo wa kuwania kufuzu bara Ulaya (Wales na washindi wa Scotland na Ukraine).