Apr 06, 2022 02:51 UTC
  • Iran: Tuko tayari kuisaidia Afghanistan kulima mazao ya chakula badala ya mihadarati

Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Afghanistan umesema kuwa, Tehran iko tayari kuisaidia Afghanistan kulima mazao ya chakula badala ya mmea wa mpopi unaozalisha mihadarati na madawa haramu ya kulevya.

Shirika la habari la ISNA limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, ubalozi wa Iran nchini Afghanistan umeelezea kufurahishwa na uamuzi wa serikali ya mpito ya kundi la Taliban wa kupiga marufuku uzalishaji, ununuaji na uuzaji wa madawa ya kulevya na umesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiisalmu iko tayari kuisaidia Afghanistan kuzalisha mazao ya chakula na yenye manufaa kwa mwanadamu badala ya mmea wa mpopi unaotumiwa kuzalisha mihadarati.

Sayyid Rasool Mousavi, Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, utekelezaji wa marufuku ya upandaji wa mmea wa mpopi huko Afghanistan utasababisha matatizo makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika nchi hiyo ambayo uchumi wake unachangiwa na uuzaji wa madawa haramu ya kulevya hivyo kuna haja ya kuweko ukulima mbadala haraka iwezekanavyo wa kuchukua nafasi ya uzalishaji wa mihadarati.

Ukulima wa mmea wa mpopi wa kuzalisha mihadarati nchini Afghanistan

 

Jumapili wiki hii, mkuu wa kundi la Taliban, Mulla Hibatullah Akhundzada alitoa amri ya kupigwa marufuku uzalishaji wa aina yoyote ile wa madawa ya kulevya huko Afghanistan.

Amri hiyo imetolewa katika hali ambayo, kwa muda wa miaka 20 ya kukaliwa kwa mabavu Afghanistan na madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani, uzalishaji wa madawa ya kulevya uliongezeka kwa kiwango kikubwa mno nchini humo kiasi kwamba asilimia 90 ya madawa ya kulevya aina ya tiryak duniani, yanazalishwa nchini Afghanistan.

Tags