Apr 06, 2022 10:44 UTC
  • Iran yapongeza marufuku ya kilimo na usafirishaji wa mihadarati kutoka Afghanistan

Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Rasoul Mousavi, Jumatatu iliyopita aliandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba:

"Marufuku ya kilimo cha mpopi nchini Afghanistan itakuwa na madhara makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika nchi hiyo na uchumi wa mweusi duniani. Uzalishaji wa afyuni ulifikia kiwango cha chini cha tani 200 mara moja tu katika miaka 32 iliyopita wakati kiongozi wa Taliban alipopiga marufuku kilimo cha mpopi; uzalishaji wa kasumba umekuwa ukiongezeka na kufikia maelfu ya tani kwa mwaka." 

Wakati kundi la Taliban lilipoidhibiti na kuitawala Afghanistan kwa mara ya kwanza, kiongozi wa kundi hilo alipiga marufuku kilimo cha mpopi, jambo ambalo lilipelekea kupungua uzalishaji wa kasumba kwa kiasi kikubwa nchini humo.

Jumapili iliyopita kundi la Taliban lilitoa amri iliyohusishwa na kiongozi wa kundi hilo, Hibatullah Akhundzada, ikitangaza kwamba kuanzia sasa "amepiga marufuku" kilimo, uzalishaji na uuzaji wa mihadarati nchini Afghanistan, na kwamba watakaokiuka amri hiyo watashughulikiwa kwa mujibu wa "sheria za Kiislamu." Amri ya kiongozi wa Taliban pia amepiga marufuku utumiaji, ununuzi na uuzaji wa mihadarati na pombe kote nchini Afghanistan.

Hibatullah Akhundzada

Katika kipindi cha miaka 20 ya uwepo wa wanajeshi wa kigeni nchini Afghanistan, nchi hiyo imeshuhudia ongezeko kubwa la uzalishaji na kilimo cha mihadarati, kwa kadiri kwamba sasa Afghanistan inahesabiwa kuwa mzalishaji mkubwa wa mihadarati duniani, ikizalisha asilimia 90 ya kasumba hiyo duniani. Kilimo na uzalishaji wa mihadarati nchini Afghanistan umekuwa ukiongezeka kwa kasi tangu 2002. Katika kipindi chote cha uvamizi wa majeshi ya Marekani na NATO nchini Afghanistan uzalishaji wa mihadarati nchini humo uliongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa licha ya madai ya nchi za Magharibi kuhusu mapambano dhidi ya kilimo na uzalishaji wa mihadarati. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinasema, mwaka 2000 uzalishaji wa dawa za kulevya nchini Afghanistan ulipungua hadi chini ya tani 200 kwa mwaka na eneo lililokuwa likitumiwa kwa ajili ya kilimo cha mihadararati lilikuwa karibu hekta 7,000; lakini baada ya uvamizi wa nchi wanachama wa NATO na Marekani uzalishaji wa dawa za kulevya nchini humo ulifikia zaidi ya tani 9,000.

Wanajeshi wa Marekani wakilinda mashamba ya kuzalisha mihadarati, Afghanistan.

Suala hili limeibua matatizo na changamoto nyingi kwa majirani wa Afghanistan, hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo hutumiwa na wafanyabiashara kama njia ya kupitisha dawa za kulevya kwenda Ulaya. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetumia gharama kubwa katika miongo michache iliyopita katika kukabiliana na uzalishaji na magendo ya dawa za kulevya, na vilevile katika kupambana na magenge ya magendo ya dawa za kulevya; na idadi kubwa ya askari na polisi wake wameuawa shahidi wakipambana na magenge hayo. Iran, ikiwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya magendo ya dawa za kulevya duniani, imewatoa mhanga mashujaa na vilema zaidi ya elfu 12 katika njia hiyo. Kwa sababu hiyo, Umoja wa Mataifa umeitaja Iran kuwa kinara wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Iran pia inaongoza duniani kwa kugundua na kunasa kiwango kikubwa zaidi cha dawa za kulevya licha ya vikwazo vya nchi za Magharibi, na imekuwa ikinasa zaidi ya tani elfu moja za dawa za kulevya kwa mwaka.

Katika mazingira ya sasa ambapo Taliban imetwaa madaraka nchini Afghanistan, udharura wa kukabiliana na uzalishaji wa madawa ya kulevya kwa kupiga marufuku kilimo cha mpopi na uzalishaji wa kasumba unahesabiwa kuwa moja ya kazi na majukumu ya haraka na muhimu ya kundi hilo, na kwa hakika ni mtihani kwa madai ya Taliban eti ya kutaka kuanzisha uhusiano mwema na wa amani unaozingatia maslahi ya pamoja na nchi jirani, ikiwa ni pamoja na Iran.

Eskandar Momeni

Eskandar Momeni, Katibu Mkuu wa Idara Kuu ya Kupambana na Mihadarati ya Iran amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha hatua yoyote ya kupunguzwa  aina zote za uzalishaji na kilimo cha mihadarati nchini Afghanistan, na imefanya na inaendelea kufanya mashauriano muhimu na jamii ya kimataifa ili kushughulikia suala la kilimo mbadala, maisha ya watu na kupunguza uzalishaji wa mihadarati nchini Afghanistan."

Tags