Iran: Israel ni dhaifu, haiwezi kuhimili nguvu za muqawama wa Palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kulaani kitendo cha wanajeshi wa Israel kuvamia viwanja vya Msikiti wa Al-Aqsa na kuvunjia heshima kibla cha kwanza cha Waislamu, amesisitiza kuwa utawala huo wa Kizayuni ni dhaifu, na wala hauna ubavu wa kustahamili nguvu za mrengo wa muqawama wa Palestina.
Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana katika mazungumzo yake ya simu na Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) na kueleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuliunga mkono taifa la Palestina.
Amesema: Hakuna shaka utawala wa Kizayuni umekuwa dhaifu mno na hauwezi kuzima mwamko wa wananchi wa Palestina na mrengo wa muqawama ambao umefanikisha operesheni za Upanga wa Quds.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza bayana kuwa, "Hii leo, muqawama upo katika hali nzuri kabisa, lakini utawala wa Kizayuni umedhoofika mno; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono kuundwa taifa moja la Palestina, mji mkuu wake ukiwa Quds."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuvunjiwa heshima Kibla cha kwanza cha Waislamu ni moja ya matokeo hasi ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, na kuna wajibu wa kuliunga mkono taifa la Palestina ambalo limesimama kidete kulinda heshima na izza ya umma wa Kiislamu.

Kwa upande wake, Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya HAMAS amesema taifa la Palestina hivi sasa linakabiliwa na machaguo mawili; ama likubali kuyahudishwa Msikiti wa al-Aqsa, au lipambane na utawala wa Kizayuni, na hakuna shaka Wapalestina na makundi ya muqawama yamekhitari njia ya mapambano.
Mamia ya wananchi wa Palestina wamejeruhiwa na kutiwa nguvuni katika hujuma mpa ya wanajeshi makatili wa Israel dhidi ya eneo hilo tukufu, mkabala wa kimya cha jamii ya kimataifa.
Wakati huohuo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kupitia taarifa limewapongeza wanamapambano wa Palestina kwa kufanya operesheni za kishujaa ambazo zimevuruga mifumo ya kiulinzi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, ushujaa ambao umegeuka na kuwa jinamizi kwa Wazayuni na waungaji mkono wao katika eneo.