Iran kuongeza ushirikiano wake wa sayansi na teknolojia na nchi za Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i8296-iran_kuongeza_ushirikiano_wake_wa_sayansi_na_teknolojia_na_nchi_za_kiislamu
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itapanua zaidi wigo wa ushirikiano wake katika masuala ya sayansi na teknolojia na nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 02, 2016 04:07 UTC
  • Iran kuongeza ushirikiano wake wa sayansi na teknolojia na nchi za Kiislamu

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itapanua zaidi wigo wa ushirikiano wake katika masuala ya sayansi na teknolojia na nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Vahid Ahmadi, Naibu Waziri wa Sayansi, Utafiti na Teknolojia wa Iran akisema hayo katika kikao cha 15 cha Baraza Kuu la kamati ya kudumu ya ushirikiano wa kisayansi na kiteknolojia ya OIC. Amesema, Iran ni mwanachama hai katika miradi ya OIC inayohusiana na teknolojia za kisasa kama teknolojia wa Nano, vyuo vikuu vya mtandaoni na vijiji vya sayansi na teknolojia. Aidha amesema, Tehran iko tayari wakati wote kupanua wigo wa ushirikiano wa utafiti wa pamoja katika masuala tofauti kama ya mazingira, elimu ya falaki na nyota na kutoa huduma za masomo kwa nchi wanachama wa OIC.

Naibu Waziri huyo pia amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono jitihada za kuimarisha ushirikiano katika masuala ya sayansi na teknolojia kati ya nchi za Kiislamu. Aidha ametoa mwito wa kufanyika jitihada za pamoja za jumuiya za kielimu za nchi za Kiislamu katika kupambana na ukosefu wa uadilifu duniani na pamoja na umaskini na kubaki nyuma kimaendeleo baadhi ya nchi za Kiislamu.