Iran yatuma ujumbe wa watu sita katika ubalozi wake mdogo nchini Saudia
Iran imetuma wajumbe wake sita wa ubalozi mdogo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje kwa ajili ya kwenda kutoa huduma kwa raia wa Iran wakati wa ibada za Hija mwaka huu.
Katika miaka ya huko nyuma, Iran ilikuwa inapeleka mahujaji 85,000 kila mwaka katika ardhi za Wahyi lakini mwaka huu idadi hiyo imepunguzwa na mamlaka za Saudia kwa zaidi ya nusu, mwaka huu mahujaji wa Iran watakuwa 40,000 tu.
Shirika la habari la ISNA limeripoti kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ndiyo inayohusika na masuala ya kibalozi ili kutoa huduma kwa raia wa Iran katika nukta tofauti duniani na kulinda haki zao. Wizara hiyo ya Mambo ya Nje ya Iran ndiyo yenye jukumu la kusimamia pia mambo yote yanayohusiana na masuala ya kidiplomasia kwa mahujaji. Hivyo karibuni hivi wanadiplomasia 6 wa Iran watatumwa huko Saudi Arabia kwa ajili ya kazi hiyo.
Baada ya kupita miaka miwili ya janga la UVIKO-19 yaani corona, mwaka huu Saudia imeruhusu idadi ndogo ya mahujaji kutoka nje ya nchi hiyo kwenda kutekeleza ibada ya Hija. Huko nyuma idadi ndogo tu ya mahujaji wa ndani ya Saudi Arabia ndio walioruhusiwa kushiriki ibada hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya Hija na Ziara ya Iran, msafara wa kwanza wa mahujaji wa Iran wataelekea kwenye ardhi za Wahyi huko Saudi Arabia kuanzia tarehe 13 Juni ambayo itasadifiana na mwezi 13 Mfunguo Pili Dhulqaad, 1443 Hijria, tukijaaliwa.