Iran: IAEA itajipotezea itibari zaidi kufuatia safari ya Grossi Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84362-iran_iaea_itajipotezea_itibari_zaidi_kufuatia_safari_ya_grossi_israel
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali hatua ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kutembelea Tel Aviv wakati huu wa kukaribia kikao cha bodi ya magavana ya shirika hilo na kuonya kuwa safari hiyo itapelekea wakala huo wa Umoja wa Mataifa kupoteza itibari zaidi.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Jun 04, 2022 03:07 UTC
  • Iran: IAEA itajipotezea itibari zaidi kufuatia safari ya Grossi Israel

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali hatua ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kutembelea Tel Aviv wakati huu wa kukaribia kikao cha bodi ya magavana ya shirika hilo na kuonya kuwa safari hiyo itapelekea wakala huo wa Umoja wa Mataifa kupoteza itibari zaidi.

Katika ujumbe wa Twitter Ijumaa usiku, Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alibainisha wasiwasi wake kuhusu kula njama IAEA na utawala haramu wa Israel. Kauli hiyo imekuja baada ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi kukutana na waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel mwenye misimamo mikali Naftali Bennet mjini Tel Aviv.

Khatibzadeh amesema Iran kama moja ya nchi za kwanza kutia saini mapatano ya NPT ya kuzuia usambazwaji silaha za nyuklia, inatoa wito kwa wote kuchukua tahadhari kuhusu kupoteza zaidi itibari ya IAEA.

Grossi amekutana na Bennet ambaye hivi karibuni amesema kuwa utawala wa Kiayuni wa Israel uko tayari kutumia nguvu za kijeshi kusitisha mpango wa nyuklia wa Iran.

Safari hiyo fupi ya Grossi mjini Tel Aviv pia imekuja baada ya ripoti mpya ya IAEA kudai kuwa, eti Iran 'haijaweka wazi' uwepo wa mada za kinyuklia katika maeneo matatu nchini.

Khatibzadeh ameashiria misimamo ya kiundumakuwili ya IAEA na kusema madola makubwa duniani hayawezi kupuuza silaha za nyuklia zinazomilikiwa na utawala wa Kizayuni na wakati huo huo kupiga kelele kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani.

Amesema hakuna anayweza kunyamaza kimya kuhusu mpango wa siri wa silaha za nyuklia wa Israel na wakati huo huo kudai kutopendelea upande wowote.