Kiongozi Muadhamu: Imam Khomeini (MA) ni roho ya Jamhuri ya Kiislamu
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameshiriki katika Hauli ya mwaka wa 33 tokea alipoaga dunia muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema, "Imam Khomeini MA alikuwa roho ya Jamhuri ya Kiislamu'
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Imam Khomeini, MA, alikuwa roho ya Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa, Imam Khomeini MA alikuwa shakhsia wa kipekee kwa maana halisi ya neno hilo. Ameongeza kuwa Imam hakuwa wa jana tu bali ni wa leo na pia ni Imam wa kesho.
Ayatullah Khamenei amelinganisha Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya mwaka 1979 na Mapinduzi ya Ufaransa ya 1789 na halikadhalika Mapinduzi ya Shirikisho la Sovieti ya 1917 na kusema, mapinduzi hayo mawili ya Ufaransa na Sovieti yalipata ushindi kwa uungaji mkono wa wananchi lakini baada ya hapo wananchi hawakuzingatiwa na waliwekwa kando na hawakuweza kushirikishwa tena katika mapinduzi ambayo wao wenyewe walijitokeza mitani kuyanga mkono na kutoa maisha yao muhanga; matokeo ya hayo ni kuwa mapinduzi hayo yaliondoka katika mkondo asili wa wananchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kinyume cha mapinduzi hayo mawili, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi kutokana na uungaji mkono wa wananchi na hata baada ya ushindi wananchi hawakutengwa. Amesema miezi mwili tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kulifanyika kura ya maoni na wananchi wakaweza kuuchagua mfumo wautakao.
Aidha amesema mwaka moja baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, uchaguzi wa kwanza wa rais ulifanyika na miezi kadhaa baadaye, uchaguzi wa kwanza wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu au bunge ulifanyika na hadi kufikia sasa karibu chaguzi 50 zimefanyika nchini tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na wananchi wamekuwa wakishiriki kwa wingi katika chaguzi hizo.
Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema maadui wanalenga kuwagonganisha wananchi wa Iran na serikali pamoja na mfumo wa Kiislamu lakini wamefeli.
Hotuba kamili ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu itawajieni katika matangazo yetu ya baadaye.