Kiongozi Muadhamu: Maadui hawataweza kuwachonganisha wananchi wa Iran na Mfumo wa Kiislamu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, katika Jamhuri ya Kiislamu, nafasi ya wananchi ni yenye umuhimu sana na maadui hawataweza kuwachonganisha wananchi na Mfumo wa Kiislamu.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika hotuba aliyotoa kwenye hauli iliyofanyika kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa 33 tangu alipoaga dunia hayati Imam Khomeini (MA).
Akihutubia umati mkubwa wa wananchi waliohudhuria hauli hiyo ambayo baada ya kupita miaka miwili imeanza kufanyika tena kwa kuhudhuriwa na watu katika haram toharifu ya Kiongozi huyo Mkuu wa Mapinduzi, Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, ni jambo la yakini kwamba, leo mapenzi ya watu kwa dini na mapinduzi ni makubwa zaidi kuliko mwanzoni mwa mapinduzi; na akalibainisha hilo kwa kutoa mifano kadhaa ya jinsi wananchi hao walivyojitokeza kwa wingi mno katika kuuenzi muqawama na wanazuoni wa kidini.
Amesema, kusindikizwa na mamilioni ya watu mwili uliokatika vipande vipande wa Shahidi Suleimani na kuenziwa mno mwanamapinduzi, mpambanaji na mujahidina huyo; na kusindikizwa na watu waliojawa na hisia kubwa za mapenzi Maraajii na Mafaqihi watajika walioaga dunia kama Ayatullah Safi Golpaigani na Ayatullah Bahjat kulikuwa kwa namna isiyoweza kulinganishwa na alivyoenziwa shakhsia yeyote wa kisiasa na wa usaniii nchini; na hilo linaonyesha itikadi na imani ya watu kwa wanazuoni, dini jihadi na muqawama.
Katika sehemu nyingie ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezifanyia uchambuzi sababu za maadui wa Iran kupanga mahesabu yao kimakosa kila mara, kwa kuashiria nafasi ya washaurii wao kadhaa ambao ni Wairani wasaliti, katika upangaji wa mahesabu na mikakati hiyo na akasema: washauri hawa mahaini hawaisaliti nchi yao pekee, bali wanawasaliti Wamarekani pia, kwa sababu, kwa kuwapatia ushauri huo potofu wanawafanya washindwe.
Halikadhalika, Ayatullah Khamenei amesema, moja ya sababu za uadui unaofanywa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ni Imam Khomeini (MA) alivyojipambanua na kujitenganisha na Wamagharibi na akalifafanua hilo kwa kusema: kuihami Palestina na kulipatia taifa la Palestina ubalozi wa utawala ghasibu wa Kizayuni na kuuokosoa waziwazi uzandiki na jinai za nchi za Ulaya na Marekani ni mifano muhimu ya jinsi Imam Khomeini alivyopambanua na kutenganisha ustaarabu, fikra na mfumo wa Kiislamu na ustaarabu na fikra ya Kimagharibi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia uharamia wa baharini ambao serikali ya Ugiriki imeifanyia Iran na akasema, siku kadhaa nyuma na kwa amri ya Marekani, Ugiriki iliiba mafuta ya Iran, lakini wakati askari mashujaa waliojitolea mhanga wa Jamhuri ya Kiislamu walipoikamata meli ya adui, zilifanywa propaganda chungu nzima za kuituhumu Iran kuhusika na wizi, ilhali ni wao walioiba mafuta yetu; na kurejesha mali iiliyoibiwia si wizi.../