Kumbukumbu za Khordad 15 kufanyika leo katika miji 900 ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84390-kumbukumbu_za_khordad_15_kufanyika_leo_katika_miji_900_ya_iran
Kumbukumbu za Khordad 15 ambazo ni maarufu kwa jina la "Mapambano ya Siku ya Allah ya Khorad 15" yanafanyika leo Jumapili katika miji 900 ya kona zote za Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 04, 2022 22:09 UTC
  • Kumbukumbu za Khordad 15 kufanyika leo katika miji 900 ya Iran

Kumbukumbu za Khordad 15 ambazo ni maarufu kwa jina la "Mapambano ya Siku ya Allah ya Khorad 15" yanafanyika leo Jumapili katika miji 900 ya kona zote za Iran.

Leo Jumapili, tarehe 5 Juni, 2022 inasadifiana na mwaka yalipotokea mapambano ya kihistoria ya Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kupambana na utawala wa kidikteta wa mfalme Shah mwaka 1963. Mapambano hayo ya mwezi Juni 1963 yalikuwa ni tukio muhimu sana katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu humu nchini na ndio uliokuwa mwanzo wa mapambano makubwa zaidi ya Kiislamu ya taifa la Iran.

Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo maafisa wa utawala wa kifalme wa Shah waliivamiaa nyumba ya Imam Khomeini MA katika mji wa Qum wa kusini mwa mkoa wa Tehran baada ya mwanachuoni huyo mwanamapambano kutoa hotuba kali ya kufichua maovu ya mfalme Shah katika madrasa ya kidini ya Faidhiya mjini Qum.

Picha ya kihistoria, sehemu ya maandamano ya wananchi wa Iran ya kumuhami kiongozi wao, Imam Khomeini MA

 

Katika hotuba yake hiyo aliyoitoa Siku ya Ashura, yaani mwezi 10 Mfunguo Nne Muhammar, Imam Khomeini MA alibainisha bila ya woga wala kificho, jinai mbalimbali za utawala huo wa kiimla wa mfalme Shah na ukibaraka wake kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Baada ya maafisa hao wa Shah kuvamia nyumba ya Imam Khomeini MA walikamata mwanmachuoni huyo kwa tamaa ya kuzima harakati zake.

Hata hivyo, hatua hiyo iliamsha hasira za wananchi ambao waliamua kusimama imara na kuanzisha harakati hiyo ya Khordad 15, mwaka 1963, na huo ukawa mwanzo wa mwamko wa Kiislamu nchini Iran ulioishia kwenye ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.

Kila mwaka wananchi wa Iran wanashiriki kwa mamilioni kwenye maandamano ya kuadhimisha tarehe hiyo muhimu sana kwao, ili kutangaza upya utiifu wao kwa Mapinduzi yao ya Kiislamu.