HAMAS: Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni tumaini la wanyonge ulimwenguni
Mjumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameashiria himaya na uungaji mkono wa kila upande wa madola ya Magharibi kwa utawala haramu wa Israel na kusema kuwa, mkabala na hilo, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamegeuka na kuwa tumaini la wanyonge ulimwenguni.
Ismail Ridhwan, afisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa kwa mnasaba wa hauli na kumbukumbu ya kuaga dunia Imam Ruhullah Khomeini (MA) muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kwamba, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mafanikio yake katika nyanja mbalimbali ulipelekea kuibuka harakati tofauti za Kiislamu katika eneo.
Kiongozi huyo wa HAMAS ameongeza kuwa, Imam Khomeini ni shakhsia ya kipekee na alikuwa na mtazama na uoni mpana kuhusiana na kadhia ya Palestina.
Kadhalika amesema kuwa, hapana shaka kuwa, sifa maalumu za shakhsia ya Imam Khomeini zilimsaidia sana katika kupata mafanikio kwenye harakati za Mapinduzi mpaka kupata ushindi mapinduzi hayo mwaka 1979 kwa uongozi wake wenye busara.
Ismail Ridhwan, afisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema pia kuwa, baada ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, taifa hili la Kiislamu limekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina na Imam Khomeini alikuqwa akiamini kwamba, Quds ndio mhimili wa mapambano na wavamizi wa Kizayuni.