Amir-Abdollahian aonya kuhusu azimio dhidi ya Iran katika IAEA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amezionya nchi ambazo zinalisukuma Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) lipitishe azimio dhidi ya Iran na kusema zitabeba dhima ya yatakayofuata hatua kama hiyo.
Katika ujumbe wa Twitter Jumapili, Amir-Abdollahian amesema Iran inakaribisha mapatano mazuri, imara na yenye kudumu kuhusu shughuli zake za Nuclear. Katika ujumbe huo ambao ameutuma baada ya mazungumzo na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borell kuhusu mazungumzo ya Vienna yanayofanyika kwa lengo la kufikia mapatano ya kuondolewa Iran vikwazo, Amir-Abdollahian ameongeza kuwa kuna uwezekano wa kufukia mapatano na nchi tatu za Ulaya ambazo ni Uingereza, Ujerumani na Ufaransa pamoja na Marekani.
Kauli hiyo imekuja siku moja kabla ya mkutano wa Bodi ya Magavana wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki. Kikao hicho kinatazamiwa kuptisha azimio dhidi ya Iran ambalo limewasilishwa na Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Marekani. Azimio hilo linatazamiwa kuituhumu Iran kuwa eti inakataa kushirikiana na IAEA.
Hali kadhalika azimio hilo linatazamiwa kupitishwa siku chache baada ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi kufika Tel Aviv na kufanya mazungumzo na wakuu wa utawala haramu wa Israel.

Hii ni katika hali ambayo utawala wa Israel ni utawala pekee unaomiliki silaha hatari za nyuklia katika eneo la Asia Magharibi. Kutokana na uungaji mkono wa Marekani na madola makubwa ya Ulaya, utawala wa Kizayuni wa Israel umekataa vituo vyake vya nyuklia vikaguliwe na IAEA mbali na kukaidi takwa la kujiunga na mkataba wa NPT wa kuzuia uundwaji na usambazjwai silaha za nyuklia.
Nchi za Magharibi na hasa Marekani zinaendeleza propaganda katika vyombo vya habari baada ya kusitishwa mazungumzo ya Vienna na zinajaribu kuonyesha kuwa eti Iran inapaswa kubebeshwa lawama za kufeli kuhuishwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA katika hali ambayo zenyewe ndizo zilizopelekea kutofikiwa mapatano kuhusu kadhia hiyo.