Watu 17 waaga dunia katika ajali ya treni ya abiria Iran
Kwa akali watu 17 wameaga dunia na makumi ya wengine kujeruhiwa kufuatia ajali ya treni ya abiria iliyotokea mapema alfajiri ya leo hapa nchini Iran.
Taarifa za awali zinasema kuwa, treni hiyo ya abiria ilikuwa ikitokea Mash'had na kuelekea katika mji wa Yazd wakati ilipotoka katika reli na kusababisha ajali hiyo. Watu 43 wamejeruhiwa katika ajli hiyo huku hali ya 16 kati yao ikiripotiwa kuwa mbaya.
Muhammad-Reza Rezei, Mkurugenzi wa Shirika la Hilali Nyekundu ya Iran katika mkoa wa Khorasan Kusini amenukuliwa akisema kuwa, ni habari ya kusikitisha kwani, watu 17 wameaga dunia katika ajali iliyotokea saa 11:30 alfajiri ya leo baada ya treni ya abiria kutoka katika reli katika eneo la Tabas yapata kilomita 50 kutoka Yazd.
Ripoti zaidi zinasema kuwa, shughuli ya kuwahamisha majeruhi na kuwapeleka hospitali ilianza mara tu baada ya kutokea ajali hiyo.
Hujjatul Islam Walmuslimin Ali Nasai Mwendesha Mashtaka wa Khorasan Kusini amesema kuwa, kutafanyika uchunguzi na kuhakikisha kuwa waliofanya uzembe na kupelekea kutokea ajali hiyo wanachukuliwa hatua za kisheria.
Afisa mmoja wa Shirika la Reli la Iran amenukuliwa akisema kuwa, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa, kugongana buldoza na treni hiyo ya abiria ndio chanzo cha ajali hiyo, ingawa amesema kuwa, ili kupata taarifa za uhakika zaidi kuhusiana na chanzo cha ajali yenyewe, wajumbe wa kamisheni kuu ya ajali wametumwa katika eneo ilipotokea ajali hiyo.
Helikopta zimeonekana zikipaa na kutua katika eneo hilo kwa ajili ya kuchukua majeruhi na kuwapeleka hospitali.