Iran yajibu kitendo cha IAEA cha kupasisha azimio lililo dhidi ya Tehran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84536-iran_yajibu_kitendo_cha_iaea_cha_kupasisha_azimio_lililo_dhidi_ya_tehran
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa, Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA imetoa azimio dhidi ya Tehran kwa kutegemea ripoti za uongo na kwa matamshi yasiyo ya kiutaalamu ya mkurugenzi mkuu wa wakala huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 08, 2022 22:38 UTC
  • Iran yajibu kitendo cha IAEA cha kupasisha azimio lililo dhidi ya Tehran

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa, Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA imetoa azimio dhidi ya Tehran kwa kutegemea ripoti za uongo na kwa matamshi yasiyo ya kiutaalamu ya mkurugenzi mkuu wa wakala huo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema pia kuwa, azimio lililopasishwa na Bodi ya Magavana ya IAEA dhidi ya Tehran imetokana na taarifa za uongo za utawala wa Kizayuni wa Israel na hatua hiyo haina matokeo mengine isipokuwa kudhoofisha tu ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wakala huo wa nyuklia.

Azimio hilo limependekezwa na Marekani pamoja na nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani na lilipasishwa jana na Bodi ya Magavana ya IAEA licha ya upinzani mkali wa China na Russia.

Bodi na Magavana ya IAEA

 

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran mapema leo Alkhamisi imetoa taarifa baada ya kupasishwa azimio hilo katika kikao cha kila msimu cha Bodi ya Magavana ya IAEA na kuongeza kuwa, Tehran inalihesabu suala hilo kuwa limefanyika kwa mashinikizo ya kisiasa ya Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, si hatua sahihi na haikubaliki hata kidogo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imesema katika taarifa yake hiyo kwamba, katika miaka iliyopita, Tehran imekuwa na ushirikiano mzuri na wakala wa nyuklia wa IAEA, na hata wakala huo umekiri mara chungu nzima kuwa, mradi wa nyuklia wa Iran ni katika shughuli zilizo wazi kabisa za amani za nyuklia kati ya wanachama wa IAEA. Pia taarifa hiyo imesema, kama ilivyotangaza huko nyuma, Tehran itachukua hatua zinazofaa za kujibu azimio hilo ambalo ni la pili kupasishwa na IAEA dhidi ya Iran tangu baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA.