Rais Raisi: Hatutarudi hata hatua moja nyuma katika msimamo wetu
Rais Ebrahim Raisi amesema Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA imepitisha azimio dhidi ya Iran lakini amesisitiza kwa kusema: "hata hivyo hatutarudi hata hatua moja nyuma katika msimamo wetu."
Azimio dhidi ya Iran lililopendekezwa na Marekani ikishirikiana na nchi tatu za Ulaya ambazo ni Uingereza, Ufaransa na Ujerumani liliwasilishwa siku ya Jumanne kwa Bodi ya Magavana ya IAEA.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema hatua ya Washington na nchi tatu za Ulaya ni kinyume na taratibu za kidiplomasia, ni ya pupa na haijengi bali itaufanya mchakato wa mazungumzo ya Vienna uwe mgumu na tata zaidi.
Nchi za Magharibi na hasa Marekani, imeamua kuendeleza kampeni yake ya propaganda za vyombo vya habari na vita vya kisaikolojia baada ya kusita mazungumzo ya Vienna ili kutafuta visingizio mbalimbali vya kutaka kuonyesha kuwa Iran ndio yenye makosa badala ya nchi hizo kutimiza ahadi na majukumu yao ili kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Akihutubia hadhara ya wananchi wa matabaka mbalimbali mkoani Chahar Mahal na Bakhtiari hapo jana, Sayyed Ebrahim Raisi amesema adui hataki Jamhuri ya Kiislamu ipige hatua kimaendeleo na akafafanua kuwa Iran imeweza kuwa na utaalamu wa nyuklia na pia utaalamu wa kisasa katika masuala ya kijeshi na ulinzi, lakini adui hataki taifa hili liwe na ujuzi na utaalamu wa kiwango cha juu.
Rais Raisi ameongezea kwa kusema: "Tunapigania maendeleo ya nchi katika vita vya irada; na vita hivi vitaendelea milele."
Katika hotuba yake hiyo, Sayyed Ebrahim Raisi vilevile amesema utamaduni wa ushindi nchini unatokana na kaulimbiu ya "sisi tunaweza" na akafafanua kwamba huo ni utamaduni wa Shahidi Qasim Suleimani, ulioiwezesha Iran kupata mafanikio mengi katika muda wa miongo minne na kupiga hatua kwa lengo la kujitegemea na kujitawala.
Seyyid Ebrahim Raisi amekumbusha pia kuwa zama za mtu kuhujumu na kuondoka zimepita na akafafanua kwamba Ugiriki iliiuzia meli moja, lakini mkabala wake zikazuiwa meli zake mbili; kwa hiyo maadui inapasa waelewe barabara kuwa watapewa jibu kali kutokana na hatua zao.../