Raisi: Mataifa ya wanamapambano yana nguvu kubwa za kusambaratisha vikwazo vya Marekani
(last modified Mon, 13 Jun 2022 03:38:33 GMT )
Jun 13, 2022 03:38 UTC
  • Raisi: Mataifa ya wanamapambano yana nguvu kubwa za kusambaratisha vikwazo vya Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hatua ya Tehran ya kutengeneza meli kubwa ya mafuta na kuikabidhi kwa Venezuela imethibitisha kivitendo kuwa mataifa ya wanamapambano yana nguvu kubwa za kuweza kusambaratisha vikwazo vya Marekani.

Meli ya pili kubwa ya mafuta iliyotengenezwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ambayo inajulikana kwa jina la Sadra ilikabidhiwa kwa Venezuela Jumamosi wiki hii mbele ya Rais Ebrahim Raisi na mwenzake Rais Nicolas Maduro wa Venezuela hapa mjini Tehran.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Rais Ebrahim Raisi ameelezea kufurahishwa sana na kuweza Iran kukabidhi kwa wakati tenda ya kutengeneza meli hiyo kubwa ya mafuta iliyotolewa na nchi ndugu na rafiki ya Venezuela na kuongeza kuwa, wakati maadui wa nchi hizi mbili wakiendelea na njama na uadui wao wa kuziwekea vikwazo vikubwa vya kiuchumi Tehran na Caracas, mataifa haya mawili ya wanamapambano yanaendelea vizuri na ushirikiano wao.

Ziara ya Rais wa Venezuela nchini Iran siku chache zilizopita

 

Amesema, hatua ya kukabidhiwa Venezuela meli kubwa ya mafuta yenye uwezo wa kubeba bidhaa zenye uzito wa tani laki moja na 13,000 (113,000) iliyotengenezwa na wataalamu wa Iran, ni mfano mzuri wa uwezo wa hali ya juu wa Iran katika kutoa huduma za kiufundi na kiuhandisi kwa mataifa mengine ulimwenguni. Pia huo ni ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha jinsi uchumi wa muqawama ulivyo muhimu na ulivyo na uwezo wa kutatua matatizo ya kila namna ya kiuchumi. 

Meli hiyo kubwa ya mafuta yenyewe ina uzito wa tani 21,500 na ni ya pili kutengenezwa na shirika la Sadra la Iran. Ina urefu wa mita 250, upana wa mita 44 na urefu wa mita 21 kwenda juu. 

Tags