Rais wa Venezuela atembelea Bustani ya Teknolojia ya Pardis nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84714-rais_wa_venezuela_atembelea_bustani_ya_teknolojia_ya_pardis_nchini_iran
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ametembelea Bustani ya Teknolojia ya Pardis iliyoko katika mji mkuu wa Iran, Tehran na kujionea ustawi mkubwa wa Iran katika sekta ya sayansi na teknolojia.
(last modified 2026-08-07T13:32:58+00:00 )
Jun 13, 2022 22:06 UTC
  • Rais wa Venezuela atembelea Bustani ya Teknolojia ya Pardis nchini Iran

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ametembelea Bustani ya Teknolojia ya Pardis iliyoko katika mji mkuu wa Iran, Tehran na kujionea ustawi mkubwa wa Iran katika sekta ya sayansi na teknolojia.

Rais Maduro ambaye aliwasili nchini Iran Jumamosi, ametembelea bustani hiyo akiwa ameandamana na ujumbe wa ngazi za juu wa mawaziri wa Venezuela wa mambo ya nje, kilimo, mawasiliano, sayansi na teknolojia, uchukizi na utalii. Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia, Sorena Sattari na mkuu wa Bustani ya Teknolojia ya Pardis waliandamana pia na Rais Maduro katika ziara yake hiyo.

Baada ya kutembelea kituo hicho cha teknolojia, Rais wa Venezuela aliwahutubu maafisa wa Iran waliokuwa hapo na kusema: "Mumeweza kutupatia motisha kutokana na uanzishaji wa mabustani ya teknolojia. Tuna hamu sana ya kuwa na miradi kama hii nchini Venezuela kwa msaada wenu."

Ujumbe huo wa Venezuela pia umetembelea mashirika ya kiteknolojia kama vile Pars Online na halikadhalika mashirika ya sekta ya kutegeneza  dawa na vifaa vya sekta ya tiba kama vile Ari Teb Firooz.

Rais Maduro akiwa katika Shirika la MAPNA

Juzi pia Rais Maduro alikabidhiwa meli kubwa ya mafuta iliyotengenezwa Iran na ambayo sasa itatumika kubeba mafuta ya Venezuela. Meli hiyo kubwa ya mafuta ina uzito wa tani 21,500 na ni ya pili kutengenezwa na shirika la Sadra la Iran. Ina urefu wa mita 250, upana wa mita 44 na urefu wa mita 21 kwenda juu.  Meli hiyo kubwa ya mafuta ina uwezo wa kubeba bidhaa zenye uzito wa tani laki moja na 13,000 (113,000) au mapipa 750,000 ya mafuta ghafi ya petroli. Meli hiyo ya kiwango cha Aframax 2 inaweza kwenda kasi ya noti 15 kwa saa baharini ambazo ni sawa na kilomita 27 kwa saa.

Jumapili, Rais Maduro pia alitembelea Shirika la Viwanda la MAPNA  ambalo linajumisha mashirika 70 ya Kiirani ambapo alipongeza ustawi mkubwa alioshuhudia wa sayansi na teknolojia katika viwanda alivyotembelea.

Rais wa Venezuela alisema MAPNA ni mfano wa namna nchi inavyoweza kusimama kidete kukabiliana na mashinikizo kwa kujitegemea.