Jenerali Ali Jafari: Israel imepata mapigo kutoka Iran lakini haisemi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84802-jenerali_ali_jafari_israel_imepata_mapigo_kutoka_iran_lakini_haisemi
Kamanda mkuu wa zamani wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amefichua kuwa Iran imetekeleza oparesheni nyingi za siri za kuushambulia utawala wa Israel lakini utawala huo umejizuia kutangaza mapigo ambayo umepata kutoka Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 16, 2022 03:47 UTC
  • Jenerali Ali Jafari: Israel imepata mapigo kutoka Iran lakini haisemi

Kamanda mkuu wa zamani wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amefichua kuwa Iran imetekeleza oparesheni nyingi za siri za kuushambulia utawala wa Israel lakini utawala huo umejizuia kutangaza mapigo ambayo umepata kutoka Iran.

Katika mahojiano na Shirika la Habari la Tasnim Jumatano, Meja Jenerali Mohamad Ali Jafari, Kamanda Mkuu wa Zamani wa IRGC amesema: "Wakuu wa utawala wa Kizayuni wanafahamu vyema mapigo waliyoyapata kutoka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Ameendelea kusema kuwa, "Baadhi ya mapigo hayo yangali yanaendelea na Wazayuni wanalengwa," na kuongeza kuwa, "Haya ni mapigo ambayo Wazayuni wamepokea kutoka harakati ya Mapambano ya Kiislamu (muqawama) katika eneo na nchi mbali mbali na hata ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel)".

Jenerali Jafari ametoa kauli hiyo baada ya taarifa za maafisa wa Israel kuhusu matukio ya hivi karibuni nchini Iran ambapo walitaka kuonyesha kuwa eti wamehusika."

Jenerali Jafari amesema, wakati Wazayuni wanapotekeleza hujuma za kigaidi, wao hutangaza wazi na mfano wa hilo ni namna walivyomuua kiwoga Shahidi Sayyad Khodaie, ndani ya gari lake akiwa mbele ya nyumba yake tena bila mlinzi.

Amesema mauaji hayo hayana thamani yoyote ya kioparesheni kwa utawala wa Kizayuni kwani mauaji kama hayo yalitekelezwa na munafikina katika muongo wa thamani, amesema, huku akiashiria kundi la kigaidi la MKO ambalo lina historia ya kutekeleza mauaji ya kigaidi dhidi ya Wairani.

Shahidi Kanali Khodaei

Kanali Khodaei, afisa wa IRGC,  aliuawa shahidi katika hujuma ya kigaidi mwezi uliopita mashariki mwa Tehran ambapo alipigwa risasi tatu kichwani na mbili mkononi.

Jenerali Jafari amesema kinyume na inavyojingamba Israel, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitangazi mapigo yote iliyousababishia utawala huo ghasibu wa Israel. Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafuata msingi wa 'kuzima taa' na usiri katika oparesheni zake dhidi ya utawala haramu wa Israel.

Kamanda huyo wa zamani wa IRGC amesema Jamhuri ya Kiislamu na harakati za muqawama zimetekeleza oparesheni kubwa dhidi ya utawala ghasibu wa Israel kabla na baad aya kuuawa Kanali Khodaei lakini maelezo hayawezi kutolewa na wananchi wanafahamu vyema sababu ya sera kama hiyo.

Jenerali Jafari amesema iwapo utawala wa Kizayuni unatekeleza oparesheni dhidi ya Iran unafahamu utapokea mapigo kadhaa ya ulipizaji kisasi.