Jun 17, 2022 03:44 UTC
  • Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki: Makelele ya kisiasa dhidi ya Iran hayaathiri chochote

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran AEOI amesema: makelele ya kisiasa na mashinikizo dhidi ya Iran hayakuwa na matokeo yoyote huko nyuma na hivi sasa pia hayatakuwa na athari yoyote.

Wakati mazungumzo ya Vienna ya kuiondolea vikwazo Iran na kurudi Marekani kwenye makubaliano ya nyuklia JCPOA yakiwa takriban yamesita kutokana na kukosekana irada ya kisiasa inayohitajika kwa upande wa Washington, kwa mashinikizo ya utawala haramu wa Israel, nchi hiyo na troika ya Ulaya inayojumuisha Uingereza, Ufaransa na Ujerumani na kwa kushirikiana na mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA Rafael Grossi zilichukua hatua ya kupitisha azimio dhidi ya Iran katika bodi ya magavana ya wakala huo.

Azimio hilo limepuuza mashirikiano makubwa na mapana iliyotoa kwa nia njema Iran kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki; na kwa sababu hiyo Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran nalo likachukua hatua ya kuondoa kamera za IAEA za uangalizi unaovuka mipaka ya usimamizi rasmi unaofanywa na wakala huo wa atomiki kwa shughuli za nyuklia za Iran.

Akizungumza na waandishi wa habari pembeni ya safari yake ya katika mji wa Natanz mkoani Esfahan hapo jana, Mkuu wa AEOI Mohammad Eslami amesema, katika muda wa miongo miwili iliyopita yamefanyika mazungumzo mengi kati ya Iran na nchi za Magharibi kuhusiana na shughuli za nyuklia za Iran zinazofanyika kwa malengo ya amani na umefanyika ukaguzi mkubwa na wa mara chungu nzima mpaka hatimaye yakafikiwa makubaliano ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA na ikaafikiwa kwamba kutokana na ukaguzi uliofanywa, faili la tuhuma zilizoibuliwa dhidi ya Iran katika kalibu ya PMD (uwezekano wa mpango wa nyuklia wa Iran kuwa na malengo ya kijeshi) lifungwe.

Eslami amebainisha kuwa, mkabala wa kufungwa faili la PMD iliafikiwa kwamba vikwazo vya kidhalimu ilivyokuwa imewekewa Iran viondolewe, na Tehran kwa upande wake ikakubali kupunguza kiwango cha shughuli zake za nyuklia sambamba na kuendelea kufanyiwa ukaguzi kwa msingi kwamba tuhuma zote za hapo kabla zitafutwa moja kwa moja na vikwazo ilivyowekewa vitaondolewa.

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amegusia jinsi upande wa pili katika makubaliano ya JCPOA ulivyohalifu kutekeleza majukumu yake na akasema: hivi sasa ambapo yamefanyika mazungumzo kwa ajili ya kurudi tena kwenye utekelezaji wa JCPOA, wameamua kuibua tena tuhuma zile zile za huko nyuma kwa kutumia nyaraka bandia za Israel, wakati Iran nayo haina sababu yoyote ya kuendelea kutekeleza majukumu yake.

Eslami amesisitiza kwa mara nyingine kuwa, faili la PMD limeshafungwa na kulifungua tena hakutawasaidia chochote.../

Tags