Rais Nicolas Maduro: Venezuela na Iran ni wahanga wa vikwazo haramu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84838-rais_nicolas_maduro_venezuela_na_iran_ni_wahanga_wa_vikwazo_haramu
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema kuwa, Venezuela na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni wahanga wa vikwazo vilivyo kinyume cha sheria.
(last modified 2026-07-02T04:13:23+00:00 )
Jun 17, 2022 03:27 UTC
  • Rais Nicolas Maduro: Venezuela na Iran ni wahanga wa vikwazo haramu

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema kuwa, Venezuela na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni wahanga wa vikwazo vilivyo kinyume cha sheria.

Rais Maduro amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar ambapo sambamba na kutoa wito wa kuweko mshikamano zaidi baina ya mataifa ya ulimwengu na taifa la Palestina amekosoa vikali vikwazo haramu vya utawala wa Marekani na washirika wake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Venezuela.

Rais Nicolas Maduro amesema kuwa: Sisi tunapendekeza diplomasia ya amani na mazungumzo; kwa hakika sisi na Iran ndio wahanga wakuu wa hatua za upande mmoja na vikwazo ambavyo kimsingi vinakinzana wazi na bayana kabisa na sheria.

Rais wa Venezuela amezungumzia pia matukio ya vita baina ya Russia na Ukraine na kueleza kwamba, madola ya Magharibi yamefanya kosa kubwa kwa kuanzisha vita vya kiuchumi na vikwazo dhidi ya Russia, kwani hatua zote hizo zinasababisha kukosekana amani na uthabiti.

 

Kuhusiana na kadhia ya Palestina, Rais Maduro amesema kuwa, nchi yake inayataka mataifa ya dunia kuwa na mfungamano zaidi na taifa la Palestina na kuongeza kuwa,  Palestina ina haki ya kuanzisha dola katika ardhi yake.

Kadhalika Rais wa Venezuela amebainisha kwamba, sisi hatuko tayari kukubali mashinikizo ya upande wowote ule kuhusiana na kadhia ya Palestina na kwamba, tutashuhudia ushindi wa malengo matukufu ya Palestina haraka au kwa kuchelewa.