Iran yaanza kutuma misaada kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i85058-iran_yaanza_kutuma_misaada_kuwasaidia_waathirika_wa_tetemeko_la_ardhi_afghanistan
Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Kabul umetangaza kuwa ndege ya kwanza yenye misaada kutoka Iran imeshawasili Afghanistan kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa mtetemko wa ardhi kusini mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Jun 22, 2022 09:14 UTC
  • Iran yaanza kutuma misaada kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Afghanistan

Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Kabul umetangaza kuwa ndege ya kwanza yenye misaada kutoka Iran imeshawasili Afghanistan kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa mtetemko wa ardhi kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Ndege hiyo yenye misaada mbali mbali imewasili nchini Afghanistan baada ya ombi la serikali ya Taliban la kutaka misaada ya kimataifa kufuatia tetemeko kubwa la ardhi nchini humo ambalo limepelekea watu takribani 1000 kupoteza maisha.

Mapema Jumatano, Ubalozi wa Iran mjini Kabul uliifahamisha Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya Taliban ya Afghanistan kuwa Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRCS)  inaweza kutoa misaada na kusaidia katika shukuli za uokoaji.

Timu za utafutaji na uokoaji na za huduma za dharura za tiba za Hilali Nyekundu ya Iran ziko tayari kuelekea Afghanistan kuwafikishia watu wa nchi hiyo misaada ya dharura.

Naye Msemaji wa Serikali ya Iran Ali Bahadori Jahromi akizungumza baada ya kikao cha baraza la mawaziri Jumatano mjini Tehran,  ametuma salamu za rambi rambi za serikali na watu wa Iran kwa familia za waathirika wa tetemeko hilo la ardhi. Jahromi amesema Iran itasimama pamoja na watu wa Afghanistan na itawapatia misaada wanayohitajia katika kipindi hiki kigumu.

Kwa upande wake, Saeed Khatibzadeh Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametuma salamu za rambi rambi kwa serikali na watu wa nchi rafiki na ndugu ya Afghanistan kufuatia tetemeko kubwa la ardhi nchini humo.

Hali baada ya mtetemeko wa ardhi nchini Afghanistan

Khatibzadeh amesema Iran iko tayari kutoa huduma za afya kwa waathirika wa zilzala hiyo.

Mapema Jumatano kulijiri mtetemeko mkubwa wa ardhi katika mikoa ya Paktika na Khost mashariki mwa Afghanistan karibu na mpaka wa nchi hiyo na Afghanistan. Mtetemeko huo uliokuwa na ukubwa 6.1 kwa kipimo cha rishta hadi sasa umepelekea watu zaidi ya 1000 kupoteza maisha.

Inasemakana kuwa idadi kubwa ya nyumba zimebomolewa na tetemeko katika eneo hilo lenye maendeleo duni.