Iran yaahidi kuisaidia zaidi Afghanistan baada ya tetemeko la ardhi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i85144-iran_yaahidi_kuisaidia_zaidi_afghanistan_baada_ya_tetemeko_la_ardhi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran iko tayari kutoa msaada zaidi wa kimatibabu kwa Afghanistan kutokana na tetemeko la ardhi lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,150 na uharibifu mkubwa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 25, 2022 03:25 UTC
  • Iran yaahidi kuisaidia zaidi Afghanistan baada ya tetemeko la ardhi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran iko tayari kutoa msaada zaidi wa kimatibabu kwa Afghanistan kutokana na tetemeko la ardhi lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,150 na uharibifu mkubwa nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka wizara ya mambo ya nje Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo alipozungumza kwa njia ya simu Ijumaa na kaimu waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Taliban Amir Khan Muttaqi.

Tetemeko la ardhi la kipimo cha 5.9 lilikumba eneo ambalo liko takriban kilomita 44 kutoka mji wa Khost mashariki mwa Afghanistan mapema Jumatano, ambalo maafisa wa eneo hilo walilielezea kuwa tetemeko baya zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika miongo miwili.

Mnamo 2002, tetemeko la ardhi la kipimo cha 6.1 liliua karibu watu 1,000 kaskazini mwa Afghanistan, na kabla ya hapo mnamo 1998 tetemeko la ardhi la kipimo cha 6.1 na mitetemeko iliyofuata kaskazini mashariki mwa Afghanistan ilisababisha vifo vya watu wasiopungua 4,500.

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya serikali na wananchi wa Iran kutokana na janga hilo kubwa, Amir-Abdollahian alisema Iran ilituma mara moja ndege mbili za mizigo zilizobeba vifaa vya huduma ya kwanza kwa jirani yake baada ya maafa hayo.

"Kama hapo zamani, tunasimama na watu wenye heshima na wenye subira wa Afghanistan," alisema, huku akiahidi kuwa Iran itaendelea kuunga mkono nchi hiyo jirani ambayo imekuwa katika mgogoro wa ndani kwa muda mrefu.

Tetemeko la ardhi Afghanistan

Hali kadhalika amesema Iran itatuma timu ya wanachama 18 ya wataalamu wa matibabu kutoka Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran kwenda Afghanistan baada ya tetemeko hilo, akisema "tuko tayari kutuma timu [nyingine] ya matibabu ikiwa itahitajika.”

Kwa upande wake kaimu waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Taliban Amir Khan Muttaqi, ametoa shukurani kwa Jamhuri ya Kiislamu kwa misimamo yake ya huruma na kutoa msaada kwa watu waliokumbwa na maafa nchini Afghanistan.

"Katika hali ya sasa, utoaji wa makazi kwa watu waliokumbwa na tetemeko ni muhimu sana," alibainisha.

Maafa hayo yanaleta changamoto mpya kwa watawala wapya wa Afghanistan na mashirika ya misaada ambayo tayari yanahangaika na majanga ya kibinadamu yanayozidi kuwa mabaya zaidi yaliyosababishwa na uwepo wa askari vamizi wa kigeni wakiongozwa na Marekani ambao waliondoka nchini humo mwaka jana.

Kulingana na mashirika ya misaada, karibu Waafghanistan milioni 19 - karibu nusu ya wakazi wa nchi hiyo - wanakabiliana na uhaba mkubwa wa chakula katika mgogoro ambao uliongezeka kwa kasi tangu majeshi ya kigeni yanayoongozwa na Marekani kuondoka Agosti iliyopita.