Aug 05, 2022 07:10 UTC
  • Sisitizo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kuhusu kuunga mkono sera ya China Moja

Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza uungaji mkono wa Iran kwa sera ya "China Moja" na kusema: 'Hatua za kichochezi za Marekani zimekuwa tishio kubwa kwa amani na uthabiti wa kimataifa.'

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliandika siku ya Jumatano ujumbe wa Twitter kwa lugha ya Kichina kufuatia ziara ya Nancy Pelosi, Spika wa Bunge la Marekani (Congress) huko katika kisiwa cha Taiwan na kusema: 'Kuheshimiwa ardhi za nchi tofauti ni mojawapo ya kanuni zinazotambulika katika sheria za kimataifa.' Amir Abdollahian amesisitiza: Uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kanuni ya China Moja hauna shaka katika uwanja huo. Vitendo vya uchochezi wa Marekani vimekuwa chanzo cha tishio kwa amani na utulivu wa kimataifa.

Tangazo la uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa sera ya China Moja limetolewa katika kuimarisha zaidi uhusiano wa Tehran na Beijing na pia kutilia mkazo upinzani wa Iran dhidi ya sera na hatua za uingiliaji za Marekani katika masuala ya ndani ya China.

Nancy Pelosi (kushoto) katika safari yake ya kichochezi katika kisiwa cha Taiwan

Chokochoko za hivi karibuni zaidi za Marekani dhidi ya China ni safari ya siri na yenye utata ya Nancy Pelosi iliyofanyika siku ya Jumanne kisiwani Taiwan. Wakati Pelosi alipokuwa anaelekea Taiwan, ndege kadhaa za kivita za China ziliruka katika eneo la Lango-Bahari la Taiwan.

Licha ya maonyo na hatua kali za China kama vile kufanya mazoezi ya anga na majini karibu na Taiwan, lakini Pelosi aliamua kufanya safari hiyo ya kichochezi ili kutangaza uungaji mkono wa Washington kwa Taiwan, licha ya kuwepo sera rasmi ya Marekani ya kutambua China Moja ambayo inajumuisha kisiwa cha Taiwan. Kwa hakika, hatua hiyo ya Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani ni uingiliaji wa moja kwa moja katika masuala ya ndani ya China na maana yake ni kuitambua Taiwan kuwa nchi huru. Pelosi ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa Marekani kuwahi kuitembelea Taiwan tangu 1997. Katika kukabiliana na uwepo wa Pelosi nchini Taiwan, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilitangaza kwamba hatua yake hiyo ni usaliti wa makusudi wa Marekani dhidi ya kanuni ya "China Moja."

Ikumbukwe kuwa kufuatia safari ya Nancy Pelosi huko Taiwan, Nasser Kanani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, kwa mara nyingine amesisitiza uungaji mkono wa Iran kwa sera ya China Moja na kulaani tabia ya Marekani ya kuibua chokochoko na mivutano duniani na kusema huko ni kuingilia masuala ya ndani ya China na kukiuka ardhi yake. Anasema: 'Kuheshimiwa ardhi za Mataifa ni moja ya misingi muhimu ya sera za nje za Iran, na kuunga mkono sera ya China Moja kunatimia katika mtazamo huo.'

Uhusiano wa Iran na China umekuwa ukiimarika katika miaka ya hivi karibuni, na hasa misimamo ya pamoja ya nchi hizi mbili katika kukabiliana na sera za kivita za Marekani, pamoja na kuanzishwa mpango wa ushirikiano wa miaka 25, inachukuliwa kuwa hatua muhimu katika mahusiano ya nchi mbili. Kuhusiana na hilo, Marais Ebrahim Raisi wa Iran na Xi Jinping wa China, katika mazungumzo yao ya simu hivi karibuni, wameeleza kuridhishwa kwao na maendeleo ya uhusiano na kuimarika kwa kasi mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi hizi mwaka uliopita. Wamekubaliana pia juu ya kuharakishwa utekelezaji wa mpango wa ushirikiano wa pande zote wa miaka 25.

Luteka ya kijeshi ya China

Kwa kutilia maanani maslahi na mitazamo yao ya pamoja kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa, Iran na China zina misingi na sababu nyingi za kukuza uhusiano wao katika nyanja tofauti. Hali na mazingira ya kieneo na kimataifa hususan kuongezeka mashinikizo ya Marekani dhidi ya China na pia siasa za uingiliaji za Washington katika eneo la Asia Magharibi na kwa upande wa pili, kuimarika zaidi kieneo na kimataifa ushirikiano wa Iran na China kumezipelekea nchi mbili hizi zihisi udharura wa kuendelea kujadiliana na kubadilishana mawazo ili kulinda maslahi yao ya pamoja.

Tags