Tehran yamlaani Biden kwa madai yake ya 'kuikomboa Iran'
Tehran imemkosoa vikali Rais wa Marekani Joe Biden kwa matamshi kuhusu kile alichodai kuwa ni ‘kuikomboa Iran’, ikisema Marekani ni mkaliaji mabavu katika historia yake na kamwe haiwezi kuwa mkombozi.
Katika chapisho kwenye akaunti yake ya Twitter siku ya Ijumaa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan'ani amesema popote pale Marekani ilipoingilia, haikuleta chochote isipokuwa mauaji, uporaji na ukosefu wa utulivu. Amesema mataifa katika eneo la Asia Magharibi na duniani kote yanashuhudia madhara ya uwepo wa jeshi la Marekani nchini Afghanistan, Iraq, Libya na Syria.
"Ukombozi wa mtindo wa Daesh unatoka kwa baba wa ubatizo wa Daesh; hakuna kingine," mwanadiplomasia huyo wa Iran ameongeza.
Biden siku ya Alhamisi aliapa kuhusu kile alitaja kuwa "kuikomboa" Iran na kusema waibua ghasia za hivi majuzi nchini Iran watafanikiwa ‘kujikomboa’ hivi karibuni.
Siku ya Ijumaa, Rais wa Iran Ebrahim Raeisi alimhutubu mtawala huyo wa Marekani na kumfahamisha kuwa Iran ilikombolewa na kupata uhuru zaidi ya miongo minne iliyopita na haitakubali tena kuwa chini ya satwa ya kibeberu ya Marekani.

"Iran ilikombolewa miaka 43 iliyopita na ina azma ya kuhakikisha haitekwi tena na Marekani wala kuwa gombe la kukamuliwa maziwa." Raisi aliyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kuadhimisha kumbukumbu ya siku ilipofanyika harakati ya kimapinduzi ya kuliteka Pango la Ujasusi la uliokuwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran mnamo Novemba 4 1979.
Siku ya Ijumaa pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian aliikosoa Ikulu ya White House nchini Marekani kwa kuunga mkono machafuko ya Iran.
Katika taarifa kupitia ukurasa wake wa Twitter, alisema rais wa Marekani anapaswa kuacha sera zake za kinafiki na uungaji mkono kwa makundi ya kigaidi kama vile Daesh.
Tokea ghasia zianze Iran wiki kadhaa zilizopita, Marekani imekuwa ikitoa taarifa za kichochezi za kuunga mkono wahuni wanaoshiriki katika ghasia hizo.