Rais Raisi: Iran, Iraq zimeazimia kupambana na ugaidi
Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesema Iran na Iraq zinatilia maanani umuhimu maalum katika kukuza amani na utulivu katika eneo, akisisitiza kuwa mataifa yote mawili yameazimia kithabiti kupambana na chanzo cha ugaidi na ukosefu wa usalama wa kieneo.
Rais wa Iran ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na Waziri Mkuu mpya wa Iraq, Mohammed Shia al-Sudani, aliyewasili mjini Tehran leo Jumanne katika ziara yake ya kwanza akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi.
Raisi amesema kuwa: "Kwa mtazamo wa Iran na serikali ya Iraq, usalama, amani na uthabiti katika eneo hili ni muhimu sana na hivyo mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi, uhalifu wa kupangwa, biashara ya madawa ya kulevya na ukosefu wowote wa usalama unaotishia eneo hili ni miongoni mwa [masuala ya] makubaliano na azma ya pamoja ya nchi hizi mbili."
Ameongeza kuwa ni nchi za eneo pekee zinazopaswa kuhakikisha usalama wa kikanda, utulivu na amani, na kusisitiza, "Uwepo wa majeshi ya kigeni katika eneo hauleti usalama hata kidogo bali ni tatizo juu ya matatizo yetu."
Aidha amesema , uwepo wa Marekani nchini Afghanistan na Iraq umeshindwa kuimarisha usalama na pia utashindwa kuleta usalama katika maeneo mengine ya eneo hili.
Rais wa Iran amesema: "Kujiondoa majeshi ya Marekani katika eneo kunaweza kuchangia sana usalama wa eneo."
Waziri Mkuu wa Iraq kwa upande wake amesema nchi yake haitaruhusu makundi ya kigaidi kutumia ardhi yake kudhuru nchi yoyote, hasa Iran.
Sudani ameongeza kuwa, usalama usiotenganishwa wa Iran na Iraq unakamilishana na ni sehemu ya usalama wa kieneo.
Amesema serikali ya Iraq iko tayari kuanzisha utaratibu wa kufanya kazi na Iran ili kuzuia mvutano wowote kwani inaamini kuwa mazungumzo na maingiliano ndio suluhisho bora zaidi la matatizo yaliyopo.
Waziri Mkuu Sudani ameashiria uwepo wa ushauri wa Iran nchini Iraq na nafasi yake katika vita dhidi ya magaidi wa Daesh na kusisitiza umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano wa pamoja wa kupambana na ugaidi na dawa za kulevya.