Kiongozi Muadhamu aitaka Iraq ilidhibiti zaidi eneo la Kurdistan lisipeleke magaidi Iran
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa, jambo lolote linalohatarisha usalama wa Iran lina madhara makubwa pia kwa Iraq na ameitaka serikali ya Baghdad kulidhibiti zaidi eneo la Kurdistan la Iraq lenye utawala wa ndani ili isiruhusu kutumiwa eneo hilo kuhatarisha usalama wa Iran.
Ayatullah Khamenei alisema hayo jana jioni wakati alipoonana na Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia’ al Sudani na ujumbe anaouongoza katika ziara yake rasmi hapa nchini Iran.
Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amempongeza al Sudani kwa kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Iraq na kusisitiza kwamba, kwa kuwa kwake Muislamu muumini, al Sudani anaweza kuiendesha na kuisimamia vizuri serikali ya Iraq.
Vile vile amesema, kati ya nchi za Kiarabu, Iraq ndiyo yenye utajiri mkubwa zaidi wa maliasili na nguvu kazi. Pia ina utajiri mkubwa na waa kale wa kihistoria, wa kiutamaduni na kiustaarabu lakini amesema, inasikitisha kuona nchi yenye utajiri wote huo na yenye hadhi ya juu kiasi chote hicho, hivi sasa haiko kenye hadhi yake hiyo. Amesema, ana matumaini wakati wa serikali ya al Sudani, Iraq itaweza kupata maendeleo, ustawi na nafasi yake ya kweli kieneo na kimataifa.
Amesema, ni wazi kwamba maadui hawataki kuiona Iraq yenye maendeleo na yenye ustawi wa hali ya juu. Hivyo inabidi kutengemea nguvu za wananchi na vijana ambao wamepasi vizuri mtihani wa kukabiliana na hatari kubwa ya genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh lilioundwa na kufadhiliwa kila kitu na maadui wa taifa hilo.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Iraq ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wake kwa serikali na wananchi wa Iraq na kusisitiza kuwa, mfano wa wazi wa ushirikiano wa karibu baina ya nchi hizi mbili ndugu ni wakati wa kupambana na magaidi wa ISIS ambapo damu za mashahidi wa Iran na Iraq zimemwagika wa pamoja kwenye mapambano hayo.
Vile vile amemtaja kwa kheri Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH aliyeuliwa kidhulma na wanajeshi magaidi wa Marekani kwa amri ya rais wa wakati huo wa nchi hiyo Donald Trump, tena akiwa uraiani nchini Iraq na kuongeza kuwa, usalama wa Iran ni usalama wa Iraq na Baghdad kamwe haitoruhusu kutumiwa ardhi ya Iraq kuhatarisha usalama wa Iran na wanchi nyingine jirani.