Khatib: Rais wa Ufaransa anaongozwa na chanzo kichafu cha CIA
Waziri wa Usalama wa Iran amezungumzia misimamo ya baadhi ya viongozi wa nchi za magharibi dhidi ya jamhuri ya kiislamu ya Iran na kjusema kuwa: Rais wa Ufaransa anaelekezwa na kuongozwa na chanzo kichafu cha shirika la ujasuusi la Marekani CIA.
Hujjatul Islam Esmaeil Khatib ambaye alikuwa akizungumza na Shirika la Habari la Iran (IRNA) ameashiria mazungumzo ya karibuni ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na baadhi ya makundi yanayoipiga vita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema: Kwa sasa hakuna tena ulazima wa Rais wa Marekani kumpa maagizo ya kufanya rais wa sasa wa Ufaransa, bali anapewa maelekezo na imla kutoka kwa maafisa wa ngazi za chini wa CIA juu ya nini anachopaswa kuseme na kufanya.
Hujjatul Islam Khatib amesema kwamba, Wamarekani wameiteka Ulaya, hasa Ufaransa na Ujerumani. Ameongeza kuwa: Japokuwa katika baadhi ya nyakati nchi za Ulaya hufanya jitihada za kutaka kuonesha alama za kuwa hai na kutokuwa tegemezi kwa Marekani kwa kuonesha msimamo, kutoa matamshi au kwa mchezo wa kidiplomasia, lakini kwa hakika alama hizo za bandia na za kipuuzi.
Waziri wa Usalama wa Iran amesema nchi zinazounga mkono fitina na machafuko nchini Iran zitakumbwa na machafuko hayo na kuongeza kuwa: Kuwepo Wamarekani katika makao makuu ya magaidi wanaotaka kujitenga katika eneo la Kurdistan nchini Iraq na kukutana kwa viongozi wa Ujerumani na magaidi hao wenye silaha wanaotaka kujitenga na Iran kutapewa majibu mwafaka.
Akiashiria vita vya Ukraine, Islam Esmaeil Khatib amesema, watu wa Ulaya wamegharamika sana kwa ajili ya mchezo huo mchafu wa Marekani, Uingereza na Wazayuni, na gharama za mgogoro huo zinatoka kwenye mifuko ya walipakodi wa Ulaya hususan Wajerumani na Wafaransa.
Waziri wa Usalama wa Iran pia ameashiria ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi za Magharibi na kusema: Kukandamizwa waandamanaji katika miji 12 ya Ujerumani, shambulio la polisi wa Canada dhidi ya mkusanyiko wa madereva wa malori nchini humo, matumizi ya silaha za nyuklia na jeshi la Marekani dhidi ya watu wa Nagasaki na Hiroshima huko Japan, uhalifu wa Marekani wa kuunda kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) na mauaji ya mamia ya maelfu ya watu katika Iraq, Syria, Libya na Afghanistan, uhalifu unaofanywa na polisi wa Marekani ndani ya nchi hiyo, mauaji na kujeruhiwa kwa waandamanaji wa Ufaransa wanaojulikana kama Harakati ya Vizibao vya Njano yanayofanywa na polisi wa nchi hiyo, mateso ya Waingereza dhidi ya watu waliokamatwa na serikali ya nchi hiyo na kukabidhiwa kwa jeshi la Marekani, misaada wa wazi wa Ufaransa na Ujerumani kwa Saddam katika vita vyake dhidi ya Iran, kuupatia silaha za kemikali utawala wa Baath wa Iraq, na uungaji mkono mkubwa kwa kundi la kigaidi la MKO, ni baadhi ya mifano ya ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na nchi hizo.