Tehran yazitaka nchi za Magharibi kutowapa hifadhi magaidi wanaoipinga Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i91484-tehran_yazitaka_nchi_za_magharibi_kutowapa_hifadhi_magaidi_wanaoipinga_iran
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imezitaka nchi za Magharibi ziache kuwapa hifadhi magaidi wanaoipinga badala ya kueneza propaganda kuhusu jibu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ghasia za hivi karibuni zinazoungwa mkono na nchi za Magharibi ndani ya nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 09, 2022 04:40 UTC
  • Tehran yazitaka nchi  za Magharibi kutowapa hifadhi magaidi wanaoipinga Iran

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imezitaka nchi za Magharibi ziache kuwapa hifadhi magaidi wanaoipinga badala ya kueneza propaganda kuhusu jibu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ghasia za hivi karibuni zinazoungwa mkono na nchi za Magharibi ndani ya nchi.

Wizara hiyo ilitoa kauli hiyo katika ujumbe wake wa Twitter siku ya Alkhamisi kujibu matamshi ya kichokozi na ya uingiliaji ambayo maafisa wa nchi za Magharibi wamekuwa wakiyachapisha kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na jibu lake halali kwa ghasia hizo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, "Katika kukabiliana na ghasia, Iran imejizuia sana - tofauti na tawala nyingi za Magharibi ambazo huwakandamiza vibaya hata waandamanaji wa amani - Iran imetumia njia za kawaida za kupambana na ghasia."

Aidha taarifa hiyo imesema mchakato wa mahakama katika kukabiliana na waandamanaji umwekuwa ni wenye kuzingatia uadilifu.

Ghasia zinazoungwa mkono na madola ajinabi zilizuka kote nchini Iran mwezi Septemba baada ya kifo cha Bi Mahsa Amini ambaye alifariki akiwa hospitalini baada ya kukamatwa na polisi.

Tukio hilo la kusikitisha lilitumiwa vibaya mara moja na watawala wa nchi za Magharibi na vyombo vyao vya kuchochea ghasia na machafuko kwa kudai kuwa eti mwanamke huyo "aliuawa" na vikosi vya polisi.

Idara ya Polisi ya Iran pia ilisambaza picha za kamera za usalama zikimuonyesha msichana huyo akiwa amezimia katika kituo cha polisi na kisha kuhamishiwa hospitalini. Idara husika nchini Iran ilifanya uchunguzi juu ya tukio hilo, na kubaini kwamba kifo cha Amini kilisababishwa na ugonjwa aliokuwa nao zamani na si kupigwa kama ilivyodaiwa.

Hali baada ya magaidi wanaopata himaya ya nchi za Magharibi kushambulia Haram ya Shah Cheragh nchini Iran hivi karibuni ambapo waumini 15 waliuawa shahidi

Mapema mwezi huu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran ilisema adui amekuwa akitumia fursa ya kadhia ya Amini kuanzisha vita vya mseto dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ili kudhoofisha mshikamano wa kitaifa na kuzuia maendeleo ya nchi. Wizara hiyo imeongeza kuwa hadi sasa watu wapatao 200 wamepoteza maisha katika ghasia hizo ambazo zinachochewa na makundi yanayotaka kujitenga na pia makundi ya kigaidi yanayopata himaya ya madola ya Magharibi na baadhi ya waitifaki wao katika eneo.

Wizara ya Mambo ya Nje iliongeza kuwa, usalama wa umma ni mstari mwekundu na kwamba mashambulio ya kutumia silaha na uharibifu hayakubaliki, hata kwa serikali za Magharibi ambazo zimeonyesha unafiki katika matamshi yao kuhusu Iran.

Taarifa hiyo ilihitimisha kwa kusema kuwa, nchi za Magharibi lazima ziache kuwakaribisha, kuwaunga mkono na kuwatia moyo magaidi," ikiashiria  hatua ya nchi za Magharibi ya kuyapa hifadhi makundi yanayopinga Iran kama vile kundi la kigaidi la MKO -- ambalo limehusika na mauaji ya kigaidi ya makumi ya maelfu ya Wairani.