Iran yazilaumu nchi za Magharibi kwa misimamo yao ya kindumilakuwili
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i91496-iran_yazilaumu_nchi_za_magharibi_kwa_misimamo_yao_ya_kindumilakuwili
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezilaumu nchi za Magharibi kwa siasa zao za nyuso mbili na za kindumilakuwili kuhusu masuala ya haki za binadamu, wanawake na uingiliaji wa mambo ya ndani wa nchi nyingine na kusisitiza kuwa, watu wanaofanya fujo, wanaofanya mauaji ya kigaidi na machafuko nchini Iran, wamekabidhiwa kwa vyombo vya sheria ili uadilifu utendeke.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Dec 09, 2022 10:04 UTC
  • Iran yazilaumu nchi za Magharibi kwa misimamo yao ya kindumilakuwili

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezilaumu nchi za Magharibi kwa siasa zao za nyuso mbili na za kindumilakuwili kuhusu masuala ya haki za binadamu, wanawake na uingiliaji wa mambo ya ndani wa nchi nyingine na kusisitiza kuwa, watu wanaofanya fujo, wanaofanya mauaji ya kigaidi na machafuko nchini Iran, wamekabidhiwa kwa vyombo vya sheria ili uadilifu utendeke.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Hossein Amir-Abdollahian akisema hayo katika mazungumzo ya simu aliyofanya na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Wopke Hoekstra, na kuongeza kuwa, kitendo cha baadhi ya viongozi na duru za Magharibi cha kutoheshimu nafasi zao na kuamua kuwachochea vijana na wanawake wa Iran na kutumia kwao vibaya vyombo vya habari kwa ajili ya kutekelezea njama zao hizo ni jambo lisilokubalika kabisa katika uga wa kidiplomasia na ndiko kulikochochea mauaji, machafuko na vitendo vya kigaidi dhidi ya wananchi wa Iran.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelalamikia vikali siasa za nyuso mbili za nchi za Magharibi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema, ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba waliofanya vitendo vya kigaidi, machafuko na uharibiru kwa kutumia silaha moto na baridi dhidi ya polisi na kuhatarisha usalama katika jamii, lazima watahukumiwa kiuadilifu kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ikumbukwe kuwa katika machafuko ya hivi karibuni yaliyotokea kwenye baadhi ya miji ya Iran, viongozi wakuu wa kisiasa wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na kwa kutumia vyombo vyao vya lugha ya Kifarsi vyenye chuki na wananchi wa Iran, vimekuwa vikiunga mkono waziwazi mauaji na machafuko hayo kwa madai ya eti kupigania haki za wananchi wa Iran. Lakini mamilioni ya wananchi wa Iran wamejitokeza mabarabarani na kwenye maeneo ya umma kutangaza uungaji mkono wao kwa mfumo wao wa Jamhuri ya Kiislamu na kulaani kwa kauli moja jinai zinazochochewa na madola ya Magharibi na vibaraka wao, ndani ya Iran.