Iran yaonya majirani juu ya visiwa vya Ghuba ya Uajemi
Naibu Spika wa Bunge la Iran amesisitiza kuwa Tehran inamiliki visiwa vitatu vya eneo la Ghuba ya Uajemi ambavyo Umoja wa Falme za Kiarabu umekuwa ukidai kuwa eti ni milki yake.
Akizungumza mwanzoni mwa kikao cha wazi cha Bunge Jumapili, Ali Nikzad amesema Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu kali kwa malengo yoyote ziada ya majirani zake.
Aidha amesisitiza kuwa siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimekuwa ni kutowatawala wengine na kutokubali kutawaliwa.
Kauli ya mbunge huyo mwandamizi imekuja kama kujibu taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya kikao cha rais wa China na viongozi wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi katika mji mkuu wa Saudia wa Riyadh tarehe 9 Disemba. Taarifa hiyo ilipinga umiliki wa Iran wa visiwa vitatu vyake vya AbuMusa, Tunb Ndogo, na Tunb Kubwa.
Nikzad alisema katika hotuba yake kwa wabunge wa Iran kwamba, "Kuthibitisha mamlaka kamili ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran juu ya visiwa hivyo vitatu hakuhitaji hata mapitio ya kisheria na mikataba ya kimataifa na nyaraka za Umoja wa Mataifa."

Akisisitiza kuwa Iran inapendelea majirani wenye ustawi, usalama na wanaostawi kiuchumi, mbunge huyo alisisitiza kuwa kuwa, "Iran haiingilii masuala ya ndani ya nchi jirani" na kuongeza kuwa "Iran kamwe haitalegeza msimamo kuhusu mipaka yake ya kitaifa."
Mbunge huyo mkuu ameitaja sera ya ujirani mwema kuwa ni itikadi thabiti katika sera ya mambo ya nje ya Jamhuri ya Kiislamu na akasema: "Iran daima imethibitishwa kuwa rafiki na muungaji mkono mkubwa wa majirani zake."
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter siku ya Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian kwa mara nyingine tena alisisitiza kuwa visiwa vitatu hivyo vya Ghuba ya Uajemi ni sehemu za milele za ardhi ya Iran na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitafanya mazungumzo kuhusu mamlaka ya mipaka yake.
Maafisa wa Iran wamesisitiza mara kwa mara kwamba visiwa vitatu vya Abu Musa, Tunb Ndogo na Tunb Kubwa ni sehemu ya ardhi yake.