Naibu Waziri Mkuu wa China amesisitiza kuwa nia na irada ya Beijing ya kustawisha uhusiano mpana wa kistratejia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitabadilika na akabainisha kwamba nchi yake inaunga mkono mamlaka ya kitaifa, umoja wa ardhi yote na heshima ya kitaifa ya Iran pamoja na msimamo wake wa kupambana na uingiliaji wa kigeni. Hu Chunhua ameyasema hayo katika mkutano na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Mohammad Mokhber.
China: Tunaheshimu mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi yote ya Iran
Dec 13, 2022 23:02 UTC
Naibu Waziri Mkuu wa China amesisitiza kuwa nia na irada ya Beijing ya kustawisha uhusiano mpana wa kistratejia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitabadilika na akabainisha kwamba nchi yake inaunga mkono mamlaka ya kitaifa, umoja wa ardhi yote na heshima ya kitaifa ya Iran pamoja na msimamo wake wa kupambana na uingiliaji wa kigeni. Hu Chunhua ameyasema hayo katika mkutano na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Mohammad Mokhber.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, katika mazungumzo ya viongozi hao yaliyofanyika mjini Tehran kupitia mkutano wa "Mpango wa Mashirikiano Kamili Kati ya Iran na China" Hu Chunhua ameashiria rekodi ya historia ya uhusiano baina ya nchi hizo mbili na akasema, Iran na China inapasa zipeane msukumo na uungaji mkono kamili katika uga wa kupambana na uingiliaji wa kigeni na kuimarisha mashirikiano na uratibu wao katika uwanja wa mapambano dhidi ya ugaidi.
Naibu Waziri Mkuu wa China ameashiria pia mpango wa miaka 25 wa ushirikiano wa pamoja kati ya Iran na China na matunda yaliyopatikana katika makubaliano baina ya pande mbili na akaongeza kuwa, mafanikio hayo ni muhimu na chanya kwa pande zote mbili, yakiwa ni matokeo ya juhudi za pamoja, na kwamba Beijing ina hamu kuimarisha ushirikiano na mashauriano baina yake na Tehran ili kuendeleza mchakato wa kustawisha uhusiano kati ya nchi mbili.
Katika mazungumzo hayo, Mohammad Mokhber, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameuelezea uhusiano kati ya nchi mbili kuwa ni wa muda mrefu na wa kihistoria na akasema, Iran na China zina mtazamo mmoja na misimamo ya pamoja katika kukabiliana na mielekeo ya ulimwengu wa kibeberu ya kujichukulia hatua za upande mmoja na kwamba mazungumzo chanya na yenye kujenga yanaendelea kufanywa na pande mbili juu ya masuala mbalimbali.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekumbusha kuwa, kulindwa na kuheshimiwa umoja wa ardhi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni suala nyeti na lenye umuhimu mkubwa kwa viongozi na wananchi wote wa Iran na akasisitiza kwamba kuna udharura kwa nchi zote kuchunga msingi huo unaohusu kila nchi na usioweza kutetereshwa.
Inafaa kuashiria kuwa, kikao cha "Mashirikiano Kamili ya Kimkakati Baina ya Iran na China" kilianza jana Jumanne kwa kuhudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Naibu Waziri Mkuu wa China hapa mjini Tehran.../