Eje'i :Shahidi Soleimani aliibua umoja wa Shia na Sunni katika nchi nyingi
Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha hatua alizochukua Shahidi Jenerali Hajj Qassem Soleimani katika medani za muqawama au mapambano dhidi ya maadui na kusema kwamba alijenga umoja kati ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni katika nchi nyingi.
Kwa mujibu wa IRNA, Hujjatul-Islam wal-Muslimeen Gholamhossein Mohseni Eje'i, Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, alisema Jumatatu katika mkutano wa 'Ukuruba wa Madhehebu, Wanazuoni na Muqawama' katika msikiti wa mji wa Kerman kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Hajj Qassem Soleimani kwamba, adui alitaka kuunda mrengo kwa jina la Uislamu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kwa msingi huo akabuni kundi la kigaidi la Daesh au ISIS na kuwahadaa vijana wengi wa Kiislamu.
Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, katika hali hiyo Waislamu wote waliungana na Jenerali Soleimani akiwa mwanajeshi wa Kiislamu katika sehemu tofauti na hivyo Shahidi Soleimani akaweza kuwavutia watu kote duniani.
Akizungumzia mienendo na maadili ya Jenerali Soleimani, Mohseni Eje'i amesema kwamba kama ambavyo adui alikuwa anatekeleza vita vya pande kadhaa, Shahidi Soleimani pia alifanya kazi za kitamaduni, kijamii, vyombo vya habari, kiintelijensia na kijeshi katika matukio yote kama kamanda wa IRGC.
Mkuu huyo wa Vyombo vya Mahakama vya Iran amesisitiza kuwa, leo hii adui bado anaogopa hata baada ya kuuawa shahidi Soleimani kwa sababu anajua kwamba mashahidi wengine kama Shahidi Soleimani wapo na wataibuka.
Luteni Jenerali Soleimani, ambaye alikuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu Kamanda wa Jeshi la Kujitolea la Wannachi wa Iraq (PMU) na wanamapambano wenzao waliuawa shahidi katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad mapema Januari 3, 2020. Shahidi Soleimani alikuwa ameelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.
Ikulu ya White House na Pentagon zilitangaza kuwa Marekani ilihusika na mauaji hayo ya kigaidi na kuthibitisha kuwa shambulio hilo lilitekelezwa kwa maelekezo ya Rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump.
Mipango mbalimbali imepangwa kutekelezwa nchini Iran, Iraq na nchi nyingine kadhaa ili kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha kishahidi cha Jenerali Soleimani, al-Muhandi na wanajihadi wenzao.