Jan 09, 2023 10:50 UTC
  • Iran kuwa mwenyeji wa nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS)

Tehran karibuni hivi inatazamiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kwanza baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS).

Hayo yamesemwa na Mehdi Safari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayesimamia Diplomasia ya Uchumi na kuongeza kuwa, mkutano huo baina ya Jamhuri ya Kiislamu na viongozi wa nchi za Afrika Magharibi utafanyika mwezi ujao wa Februari.

Safari amesema hayo katika mkutano wa 16 wa Uratibu wa Uhusiano wa Kiuchumi wa Kigeni, ambao umechunguza na kutathmini uhusiano wa Iran ya Kiislamu na nchi za magharibi mwa Afrika.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, mkutano huo baina ya Iran na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) utafanyika kwa kuzingatia uhusiano wa karibu wa Tehran na nchi hizo za Kiafrika katika nyuga za madini, kilimo, na biashara.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amebainisha kuwa, soko na jamii kubwa ya watu wa nchi za Afrika Magharibi vinatoa fursa kwa Iran kuwekeza na kuuza bidhaa zake katika mataifa hayo, hususan huduma za teknolojia na uhandisi.

Ramani na bendera za nchi wanachama wa jumuiya ya ECOWAS

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayesimamia Diplomasia ya Uchumi wa Iran ameongeza kuwa, mbali na kuwa mwenyeji wa viongozi wa ECOWAS mwezi Februari, lakini Iran pia karibuni hivi itafanya kikao na kamisheni za uchumi za Senegal na Ivory Coast.

Aidha katika mkutano huo wa 16 wa Uratibu wa Uhusiano wa Kiuchumi wa Kigeni wa Iran, Jamhuri ya Kiislamu imesaini makubaliano 13 ya maelewano baina yake na Cuba, katika nyuga za sayansi, afya, teknolojia, nanoteknolojia, uhandisi, biashara, michezo, elimu na uhusiano wa kibenki.

 

Tags