Raisi: Shahidi Soleimani, IRGC mashujaa wa vita dhidi ya ugaidi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza rekodi ya kuvutia ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika vita dhidi ya ugaidi na kusema kuwa, Luteni Jenerali Qassem Soleimani ni nembo na shujaa wa mapambano dhidi ya magenge ya kigaidi katika eneo la Asia Magharibi.
Rais Ebrahim Raisi alisema hayo jana katika mkutano wake na makamanda wa IRGC katika mkoa wa Azerbaijan Magharibi, kwa mnasaba wa Siku ya Taifa ya Walinzi na kuongeza kuwa, vikosi vya usalama vya Iran daima vimedhamini usalama na kuvunja njama na nyendo ovu za maadui katika eneo.
Sayyid Raisi amesema maadui wanatiwa wahaka na kuviogopa vikosi vya SEPAH, kwa kuwa jeshi hilo la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu siku zote linalinda thamani za kiroho, taifa la Iran na nchi hii kwa ujumla.
Rais wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kumuenzi Shahidi Soleimani, ambaye ni nembo ya kimataifa ya mapambano dhidi ya madola yenye kiburi na ugaidi. Amesema Shahidi Soleimai alipambana na kusimama kidete dhidi ya ukandamizaji na dhulma za mfumo wa kibeberu duniani.
Rais Raisi amebainisha kuwa, "Ubeberu wa dunia uliunda Daesh na magenge mengine ya kigaidi, lakini uwepo wa jeshi la IRGC umepelekea kudhaminiwa usalama katika eneo."
Jenerali Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Naibu Kamanda Jeshi la Kujitolea la Wannachi wa Iraq (PMU) Abu Mahdi al-Muhandis, na wanamapambano wenzao waliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad Januari 3, 2020. Shahidi Soleimani alikuwa ameelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, Shahidi Soleimani aliweza kuhuisha utambulisho wa Kiislamu katika eneo hili na daima ataendelea kuenziwa kwa mchango wake katika vita dhidi ya ugaidi.