Iran yakaribisha hatua ya Waarabu ya kuhuisha uhusiano na Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94578-iran_yakaribisha_hatua_ya_waarabu_ya_kuhuisha_uhusiano_na_syria
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepongeza hatua ya nchi za Kiarabu ya kuhuisha na kuimarisha uhusiano na Damascus, akisisitiza kuwa mkondo huo mpya wa kurejea mataifa ya Kiarabu nchini Syria unaonyesha kuporomoka kwa njama za nchi za Magharibi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 28, 2023 23:10 UTC
  • Iran yakaribisha hatua ya Waarabu ya kuhuisha uhusiano na Syria

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepongeza hatua ya nchi za Kiarabu ya kuhuisha na kuimarisha uhusiano na Damascus, akisisitiza kuwa mkondo huo mpya wa kurejea mataifa ya Kiarabu nchini Syria unaonyesha kuporomoka kwa njama za nchi za Magharibi.

Nasser Kan'ani amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana Jumanne na kuongeza kuwa, kitendo cha Waarabu cha kuikumbatia tena Syria baada ya kuitenga kwa zaidi ya muongo mmoja ni hatua nzuri itakayaochangia kuimarika umoja na mshikamano wa umma wa Kiislamu.

Juzi Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Shoukry, aliitembelea Damascus kwa ziara ya kikazi na kuonana na Rais Bashar al Assad. Hiyo ni ziara ya kwanza ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri nchini Syria tangu miaka 12 iliyopita wakati taifa hilo la Kiarabu lilipovamiwa na magenge ya kigaidi kwa msaada wa madola ya Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu.

Nchi za Saudi Arabia na Muungano wa Falme za Kiarabu zilishinikiza kusimamishwa uanachama wa Syria ndani ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ili kuonesha uungaji mkono wao wa wazi kwa magenge ya kigaidi na kikatili yaliyomiminwa kufanya jinai huko Syria.

Aidha Jumapili iliyopita, Maspika wa Mabunge ya nchi za Kiarabu walienda nchini Syria ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 12 iliyopita. Baada ya ziara hiyo ya kihistoria, Spika wa Bunge la Misri, Hanafy Ali El-Gebali, alisema kuwa, Syria itarejea kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League).

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, "Maendeleo ya karibuni katika uhusiano wa nchi za Kiarabu na Syria, ikiwemo ziara ya ujumbe wa Mabunge ya Kiarabu mjini Damascus ili kuonyesha mshikamano na Wasyria kufuatia janga la mitetemeko ya ardhi, ni hatua chanya katika kuelekea kwenye umoja wa Waislamu."

Kan'ani ameongeza kuwa, iwapo nchi hizo zitatazama mambo kwa uhalisia wake, ziungane, zifanye maamuzi huru na kujiepusha na ubeberu wa maajinabi, hakuna shaka kuwa nchi za eneo hili zitaweza kusuluhisha matatizo yao kupitia mazungumzo na mikakati ya kieneo.