Eslami: Wamagharibi wameikubali Iran ya nyuklia
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema kuwa leo hii Wamagharibi wameikubali Iran kuwa nchi yenye nishati ya nyuklia na kusisitiza kuwa, chaguo pekee lililobakia kwa Magharibi ni kukabiliana na Iran kidiplomasia.
Wataalamu na wanasayansi vijana wa Iran, wamepiga mafanikio makubwa katika teknolojia ya nishati ya nyuklia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Mohammed Eslami alisema hayo jana Alkhamisi na kuongeza kwamba, kuweza kuwa na nguvu za kiuchumi pembeni mwa nguvu za kielimu na kiteknolojia, hulizawadia taifa uhuru kwa maana halisi ya neno.
Mkuu huyo wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) ameongeza kwamba, kama tutakuwa na nguvu amilifu za kielimu na kiteknolojia na tukaendelea nazo muda mrefu sambamba na kuimarisha mashirika ambayo msingi wake ni elimu, bila ya shaka yoyote tutaweza kufikia vilele vyote vya mafanikio.
Ameongeza kuwa, kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hadi leo hii, maadui kamwe hawakuwa tayari kuifanya Iran imiliki teknolojia ya nyuklia ukiwemo mchakato mzima wa fueli nyuklia, lakini leo wamelazimika kuikubali Iran ya nyuklia kwani vijana wa Iran wamefanikiwa kumiliki teknolojia hiyo. Amesema, bila ya shaka sababu kuu ya vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ni kuvunja mori na moyo huyo wa wananchi wa Iran.
Vilevile amesema, Wamagharibi hivi sasa wameelewa kuwa hawana chaguo jingine la kuamiliana na Iran ya Kiislamu isipokuwa njia za kidiplomasia. Amesema, kama Iran isingekuwa na teknolojia ya nyuklia isingeweza kutoa matibabu kwa kutumia teknolojia hiyo ambayo faida zake kuu ni za kimatibabu.