Abdollahian: Umefika wakati vikosi vamizi viondoke Syria mara moja
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema vikosi vya nchi ajinabi vinapaswa kuondoka katika ardhi ya Syria haraka iwezekanavyo.
Hossein Amir-Abdollahian ametoa mwito huo katika kikao na waandishi wa habari mjini Damascus akiwa pamoja na mwenzake wa Syria, Faisal Mekdad na kusisitiza kuwa, vikosi ajinabi vinatishia usalama na mamlaka ya kujitawala ya Syria, na vinapaswa kuondoka nchini humo mara moja pasi na masharti yoyote.
Kadhalika amelaani hatua ya jeshi la Marekani na vibaraka wao ya kupora mafuta, nafaka na rasilimali nyinginezo za Wasyria huko mashariki na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Kiarabu, na kubainisha kuwa wizi huo unakiuka wazi Hati ya Umoja wa Mataifa.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza bayana kuwa, mgogoro wa Syria hauwezi kumalizwa bila kukomesha ukaliaji wa mabavu wa ardhi ya nchi hiyo, sanjari na kukabiliana na magenge ya kigaidi. Amewataka wavamizi kuheshimu uhuru, mamlaka ya kujitawala, usalama na uthabiti wa Syria na eneo zima la Asia Magharibi.
Aidha Waziri wa Mashauri wa Kigeni wa Iran amesema vikosi vamizi vya kigeni vinapasa kuhitimisha chokochoko na hatua zao za uvamizi dhidi ya mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Syria.
Hapo jana katika mazungumzo yake na Rais Bashar al-Assad wa Syria mjini Damascus, Amir-Abdollahian alilaani wimbi la mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria na kusisitiza kuwa, mashambulizi hayo ya Wazayuni yanakinzana waziwazi na sheria za kimataifa kuhusu masuala ya kibinadamu na wakati huo huo yanauweka hatarini usalama na amani ya kikanda na kimataifa.
Abdollahian ameongeza kuwa, kitendo cha Wazayuni cha kushambulia Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Allepo (Halab) wakati huu ambapo taifa hilo linakabiliwa na matatizo chungu nzima kutoka na maafa makubwa ya matetemeko ya ardhi, kinaonesha dhati ya ukatili wa utawala huo bandia.