Iran yakosoa undumakuwili wa Ufaransa juu ya suala la haki za binadamu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani undumakuwili wa Ufaransa, ambayo kwa upande mmoja inajinadi kuwa mbeba bendera ya kutetea haki za binadamu, lakini kwa upande wa mwngine inakanyaga haki hizo kwa vitendo.
Huku akiashiria kukandamizwa maandamano ya wananchi Ufaransa, Nasser Kan'ani ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, Ufaransa haitekelezi kile 'inachohubiri' ikija katika suala la haki za binadamu.
Kana'ani ameeleza kuwa, kushambuliwa waandamanaji nchini Ufaransa wakifanya maandamano ya amani ni mfano mwingine wa namna haki za binadamu 'zinavyoheshimiwa' katika 'Bustani la Ulaya'.
Hapo jana, askari polisi nchini Ufaransa waliwashambulia vibaya maelfu ya watu wanaoshiriki maandamano ya kulalamikia sera za Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo, na hususan mageuzi tata ya pensheni yaliyotazamiwa kuanza kutekelezwa mwaka huu wa 2023.
Polisi ya Ufaransa iliwashambulia waandamanaji kwa mabomu ya gesi ya kutoa machozi na risasi za mipira, ambapo baadhi yao wamelazwa hospitalini kutokana na majeraha.

Wafanyakazi nchini Ufaransa wanalalamikia hatua ya Seneti kupasisha muswada wa kuongeza umri wa kustaafu kutoka umri wa miaka 62 ya sasa hadi miaka 65 katika sheria hiyo tatanishi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, watu ambao ndio wakiukaji wakubwa wa kila siku wa haki za binadamu ulimwenguni, leo hii wanajifanya kuwa wabeba bendera na watetezi wa haki za binadamu.