Iran na Imarati zatilia mkazo kustawisha ushirikiano baina yao
Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) wamesisitiza umuhimu wa kupanua ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali.
Sisitizo hilo limo katika mazungumzo ya simu ya Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mwenzake wa Imarati Sheikh Abdullah bin Zayed al-Nahayn ambapo wawili hao wamebadilishana mawazo pia kuhusu na masuala ya pande mbili, kieneeo na kimataifa.
Huku akimpongeza na kumpa mkono wa kheri na Baraka mwenzake wa Imarati kwa kuwadia sikukuu ya Eidul-Fitr, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uhusiano uliopo baina ya Tehran na Abu Dhabi uumo katika hali ya kupiga hatua.

Aidha amesema, mikutano na mashauriano ya kina yanaendelea baina ya maafisa wan chi hizo mbili.
Sheikh Abdullah bin Zayed al-Nahay, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Imarati amesema kuhusiana na mazingira mapya yanayotawala katika eneo la Asia Magharibi na kusema kuwa, katika majuma ya hivi karibuni kumeshuhudiwa kuimarika ushirikiano katika eneo hili yakiwemo mahusiano mazuri kati ya Iran na Saudi Arabia bila kusahau na mazingira na ukurasa mpya uliofunguliwa katika uhusiano na taifa la Syria.
Aidha katika mazungumzo yao hayo, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) wamesisitiza umuhimu wa kupanua ushirikiano wa pande mbili kadiri inavyowezekana ikiwemo sekta binafsi.