Raisi: Kusimama kidete mataifa ya Syria na Palestina kumeiimarisha kambi ya muqawama
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i96980-raisi_kusimama_kidete_mataifa_ya_syria_na_palestina_kumeiimarisha_kambi_ya_muqawama
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kusimama imara mataifa ya Palestina na Syria kumebadilisha hali ya mambo kwa manufaa ya kambi ya muqawama na leo hii utawala wa Kizayuni wa Israel ni dhaifu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
May 04, 2023 03:24 UTC
  • Raisi: Kusimama kidete mataifa ya Syria na Palestina kumeiimarisha kambi ya muqawama

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kusimama imara mataifa ya Palestina na Syria kumebadilisha hali ya mambo kwa manufaa ya kambi ya muqawama na leo hii utawala wa Kizayuni wa Israel ni dhaifu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Sayyid Ebrahim Raisi ambaye yuko ziara nchini Syria amesema hayo wakati alipohutubia Waislamu ndani ya Haram ya Bibi Zainab SA mjini Damascus. 

Amesema, maadui wa Uislamu wamefanya njama na fitna kwa muda wa miaka 12 na wamemimina fedha nyingi haramu kuyasaidia magenge ya kikatili na kigaidi kama Daesh (ISIS) kama ambayo wametumia pia mabanda makubwa ya propaganda ya kibeberu dhidi ya taifa linalodhulumiwa la Syria, kuua watoto na wanawake wa taifa hilo na kuharibu miji na nyumba zao, lakini hivi sasa Syria imeibuka mshindi na imezidi kuwa imara. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, leo hii Syria inatembea kifua mbele huku maadui wa Uislamu wakiwa na kovu la milele la aibu na fedheha.

Amesema, pembeni mwa jinai za miaka 12 za Marekani na Wazayuni huko Syria na Iraq, kuna ukurasa mwingine uliojaa nuru, nao ni ukurasa wa muqawama, kusimama kidete, kujihami vilivyo mataifa hayo na kukata mikono michafu ya mabeberu ambako kumeifanya kambi ya muqawama kuwa imara zaidi.

Rais Raisi aidha amesema, wakati nchi mbili za Kiarabu na Kiislamu za Syria na Iraq zilipovamiwa na kuhujumiwa na magenge ya ukufurishaji, baadhi ya watu walishindwa kutoa tathmini sahihi, lakini Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alitoa tathmini sahihi kabisa ya njama hizo na kusema kuwa jinai hizo za Wazayuni zitashindwa, na kambi ya muqawama itazidi kuwa imara.