"Waliomzatiti kwa silaha Saddam wanatiwa kiwewe na uwezo wa kiulinzi wa Iran"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i98014-waliomzatiti_kwa_silaha_saddam_wanatiwa_kiwewe_na_uwezo_wa_kiulinzi_wa_iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu kile kilichotajwa kuwa 'wasiwasi' wa nchi za Magharibi juu ya ustawi na mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu katika uga wa ulinzi na kusisitiza kuwa, madola hayo yanayotiwa kiwewe na uwezo mkubwa wa kiulinzi wa Iran ndiyo yaliyomshajiisha na kumzatiti kwa silaha dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein ili awashambulie Wairani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 27, 2023 01:48 UTC

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu kile kilichotajwa kuwa 'wasiwasi' wa nchi za Magharibi juu ya ustawi na mafanikio ya Jamhuri ya Kiislamu katika uga wa ulinzi na kusisitiza kuwa, madola hayo yanayotiwa kiwewe na uwezo mkubwa wa kiulinzi wa Iran ndiyo yaliyomshajiisha na kumzatiti kwa silaha dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein ili awashambulie Wairani.

Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana Ijumaa, Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa, ni kinaya kwa madola hayo kujifanya kuwa yametiwa hofu na mafanikio ya kiulinzi ya Iran, katika hali ambayo ndio wauzaji wakubwa wa silaha katika eneo la Asia Magharibi.

Kan'ani amesema katika ujumbe huo kwamba: Serikali za Magharibi, hususan Marekani na Ufaransa zilikuwa na nafasi kubwa katika kuuchochea na kuumiminia silaha utawala wa Saddam Hussein katika uvamizi wake wa kijeshi na mashambulizi ya makombora dhidi ya raia ambao hawakuwa na ulinzi wa Iran.

Amesema inashangaza kuwaona Wamagharibi wanahamakishwa na mafanikio ya Iran katika sekta ya ulinzi, ilhali wenyewe wanaendelea kurundika silaha zao katika baadhi ya nchi za eneo la Asia Magharibi.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Jumatano iliyopita, kombora la Khorramshahr 4 lililopewa jina la "Khaiber" lilizinduliwa rasmi kama bidhaa mpya kabisa ya makombora yaliyoundwa na sekta ya viwanda vya anga ya Wizara ya Ulinzi ya Iran.

Kombora hilo la kistratejia lililoyatiwa kiwewe madola ya Magharibi lilizinduliwa kwa mnasaba wa maadhimisho ya tarehe 3 mwezi Khordad ambayo ni siku ya kukumbuka tukio la kukombolewa mji wa Khorramshahr, mkoani Khuzestan kusini magharibi mwa Iran.

Kufuatia uzinduzi huo, Matthew Miller, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alidai kuwa, kuendelea Iran kuimarisha makombora yake ya balestiki eti ni tishio kwa usalama wa eneo na dunia.