Iran: Tupo tayari kuisaidia Mali kukabiliana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i98198-iran_tupo_tayari_kuisaidia_mali_kukabiliana_na_ugaidi
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kuipa Mali uzoefu ilionao katika kukabiliana na ugaidi.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
May 30, 2023 05:59 UTC
  • Iran: Tupo tayari kuisaidia Mali kukabiliana na ugaidi

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kuipa Mali uzoefu ilionao katika kukabiliana na ugaidi.

Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani, Waziri wa Ulinzi wa Mali amesema hayo katika mazungumzo yake na mwenzake wa Mali, Kanali Sadio Camara hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Iran inaweza kuipa nchi hiyo ya Afrika Magharibi silaha na zana za kivita katika makabiliano yake na makundi ya kigaidi.

 Jenerali Ashtiana amesisitiza kuwa, serikali ya awamu ya 13 ya Rais Ebrahim Raisi inafanya kila iwezalo kukuza na kustawisha zaidi ushirikiano wake na nchi za Afrika ikiwemo Mali katika uga wa ulinzi.

Tangu mwaka 2012 nchi ya Mali imekumbwa na hujuma na mashambulizi ya wanamgambo wenye misimamo mikali. Nchi hiyo inaongozwa na serikali ya kijeshi kufuatia mapinduzi yaliyojiri nchini humo mwaka 2020 na 2021. 

Mali inavyosumbuliwa na ukosefu wa usalama

Kadhalika Waziri wa Ulinzi wa Iran ameipongeza Mali kwa kuiunga mkono Palestina, akisisitiza kuwa huo ni mfano hai unaoonesha kuwa taifa hilo la Kiafrika linawatetea na kuwaunga mkono wanaodhulumiwa duniani.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Mali, Kanali Sadio Camara amesema nchi yake ina hamu ya kustafaidi na uzoefu wa Iran katika vita dhidi ya ugaidi.

Kanali Camara ameeleza bayana kuwa, Mali inavutiwa na stratejia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuwatumia wananchi na vikosi vya kujitolea katika kujidhaminia usalama wake.