Iran yalaani shambulizi la bomu lililoua, kujeruhi makumi msikitini Afghanistan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani shambulio la kigaidi lililotokea jana huko Afghanistan na kuua na kujeruhi makumi ya watu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, Nasser Kan'ani amesema, Tehran inalaani kitendo chochote cha kigaidi ambacho kinahatarisha usalama wa nchi na wananchi wa Afghanistan.
Kadhalika amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa serikali, kwa wananchi wa Afghanistan na familia za wahanga wa shambulio hilo lililolenga waumini waliokuwa msikitini huko kaskazini mashariki mwa nchi.
Aidha Kan'ani amewaombea dua na maghfira ya Mwenyezi Mungu wote waliouawa kwenye shambulio hilo la kigaidi, kama ambavyo amewaombea pia afueni ya haraka majeruhi.
Hapo jana, watu wasiopungua 16 waliuawa na makumi ya wengine walijeruhiwa baada ya kutokea shambulio la kigaidi katika msikiti mmoja mkoani Badakhshan, kaskazini mashariki mwa nchi.
Shambulio hilo lililenga watu waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya kumuenzi na kumkumbuka afisa wa Taliban aliyeua katika shambulizi jingine Jumanne iliyopita. Hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo la jana.
Nissar Ahmad Ahmadi, Naibu Gavana wa mkoa wa Badakhshan aliuawa katika shambulio la bomu dhidi ya gari lililokuwa limembeba mkoani hapo. Kundi la ISIS lilikiri kutekeleza hujuma hiyo ya Jumanne.