Dec 02, 2023 04:20 UTC
  • Nukta nne za kistratijia katika matamshi ya Kiongozi Muadhamu kuhusu Asia Magharibi na kadhia ya Palestina.

Akizungumza siku ya Jumatano tarehe 29 Novemba katika kikao na askari wa kujitolea mashuhuri kama Basij kutoka pembe zote za nchi, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amegusia nukta kadhaa muhimu kuhusu operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa na stratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na kadhia ya Palestina.

Nukta ya kwanza katika matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na eneo la Asia Magharibi ni kufafanuliwa njama za Marekani dhidi ya eneo hili kupitia mpango wake eti wa Mashariki ya Kati Kubwa. Kupitia mpango huo, mifumo ya kisiasa katika nchi 6 za Iraq, Syria, Lebanon, Libya, Sudan na Somalia ilipaswa kuondolewa na kuwekwa mahala pake mifumo mipya ya kiutawala. Moja ya malengo ya mpango huo lilikuwa ni kutoa pigo kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mhimili wa muqawama, lakini si tu kuwa mpango huo wa Mashariki ya Kati Kubwa haukufaulu, bali pia siasa za Marekani katika eneo la Asia Magharibi nazo zimefeli na licha ya Marekani kutumia pesa nyingi kwa madhumuni ya kuufanikisha lakini nafasi ya nchi hiyo ya kibeberu katika eneo hili imedhoofika na nafasi ya mrengo wa mapambano kuimarika zaidi.

Sehemu ya kikao cha Basij na Kiongozi Muadhamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusiana na suala hilo: "Mashariki ya Kati Mpya inatofautiana kwa digrii 180 na hali ya hivi sasa... Mpango na njama hiyo katika eneo ilivunjwa na nguvu kubwa na yenye ufanisi ya Jamhuri ya Kiislamu, ambapo nembo na bendera ya nguvu hiyo kubwa, ilibebwa na mtu aliyeitwa Haj Qasim Soleimani, hivyo sasa inabainika wazi ni kwa nini jina la Haj Qasim ni maarufu na linapendwa sana na watu wa Iran na kuwakera maadui ...Ndio, jiografia ya kisiasa ya eneo hili inapitia mabadiliko ya kimsingi, lakini sio kwa faida ya Marekani, lakini ni kwa faida ya mrengo wa mapambano. Ndio, ramani ya jiografia ya kisiasa ya Asia Magharibi imebadilika, lakini kwa manufaa ya muqawama; muqawama ndio uliopata ushindi."

Nukta ya pili katika matamshi ya Kiongozi Muadhamu ambayo pia ilishabihiana na nukta ya kwanza, ni kwamba, matukio ya eneo hili yanaelekea kwenye mkondo wa kufutwa Marekani katika eneo, ambapo Kimbunga cha al-Aqsa ni tukio muhimu katika muktadha huu. Marekani imekuwa ikijaribu kulidhibiti eneo hili, lakini leo juhudi nyingi zinafanyika kwa shabaha ya kukabiliana na suala hilo. Kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, kupingwa udhibiti wa Marekani sio kukata uhusiano wa kisiasa na nchi hiyo, bali ni kupinga ubeberu wake, jambo ambalo limeshika kasi katika eneo. Kuhusiana na hilo, Ayatullah Khamenei amesema: "Dalili ya wazi ya kukabiliana na ubeberu wa Marekani katika eneo ni tukio la kihistoria la Kimbunga cha al-Aqsa, ambalo, ingawa limetekelezwa dhidi ya utawala wa Kizayuni, lakini ni katika mwelekeo wa kukabiliana na Marekani kwa sababu limevuruga mahesabu ya Marekani katika eneo, na iwapo litadumishwa bila shaka litafutilia mbali siasa za Marekani katika eneo hili."

Nukta ya tatu katika matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ni kukanusha hali mbili bandia na za kutwishwa na kutilia mkazo hali mbili halisi zinazotawala katika eneo hii leo. Maadui wa ulimwengu wa Kiislamu daima wamejaribu kulazimisha mifarakano ya uwongo na bandia kama vile Waarabu na wasio Waarabu, Mashia na Masunni dhidi ya eneo, na kufuatilia siasa na maslahi yao kupitia mkakati wa "gawanya utawale." Kwa maneno ya Kiongozi wa Mapinduzi, siasa hizo za kutenganisha mataifa ya eneo katika msingi wa uwili hasimu zimeshindwa kabisa na leo uwili pekee uliobakia katika eneo ni uwili wa muqawama kwa upande mmoja na wa kudhilalisha na kusalimu amri mbele ya maadui kwa upande wa pili. Kiongozi Muadhamu amesema kuhusiana na hilo: "Migawanyiko hii yote ya kulazimishwa imesambaratika na sasa kuna uwili mmoja mpya unaotawala katika eneo; uwili wa muqawama na wa kujisalimisha. Leo ni uwili huu mmoja ndio unaojadiliwa katika eneo. Muqawama ni kutojisalimisha mbele ya siasa za mabavu, ubeberu na uingiliaji wa Marekani."

Mabasij wengine waliohudhuria kikao hicho

Nukta ya nne ya kistratijia katika matamshi ya Kiongozi Muadhamu hapo siku ya Jumatano ni kutilia mkazo kwa mara nyingine udharura wa kufanyika kura ya maoni kuhusu suala la Palestina. Huku akionyesha matumaini ya kuanzishwa taifa la Palestina, Kiongozi wa Mapinduzi amekanusha madai ya nchi za Magharibi kwamba Iran inajaribu kuwaangamiza Mayahudi na kueleza kuwa kubuniwa taifa la Palestina kunatokana na stratijia ya kimantiki na ya kudumu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo inasisitiza juu ya kufanyika kura ya maoni kati ya Wapalestina wote. Kutilia mkazo stratijia hii, mbali na kukanusha tuhuma za eti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuwaangamiza Mayahudi, ni jambo lenye umuhimu mkubwa wakati huu. Hii ni kwa sababu nchi za Magharibi zinajaribu kupandikiza chuki na kueneza uvumi kuhusu Uyahudi katika suala la Palestina na Israel, na hivyo kufunika ubandia wa utawala huo pamoja na kukataa kwake kushiriki katika kura ya maoni kuhusiana na mustakbali wa ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.

Tags