Feb 18, 2024 09:32 UTC
  • Vitisho vipya vya wakosoaji wa Natenyahu; Kuvunjwa Baraza la Mawaziri la Vita

Sambamba na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu kuendeleza tabia yake ya kujichukulia hatua za upande mmoja, wakosoaji wake wametishia kulivunja Baraza la Mawaziri la Vita la utawala huo.

Moja ya matokeo muhimu ya kuendelea vita vya Gaza ni kujitokeza na kushtadi hitilafu na mivutano katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel na ndani ya Baraza la Mawaziri la Vita la Natenyahu.

Watu katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu wanalalamikia kutojali Netanyahu na baraza lake la mawaziri hali na hatima ya mateka wanaoshikiliwa na Hamas na vilevile athari zinazohisika za kiuchumi za vita na wamekuwa wakibainisha malalamiko yao kwa kufanya maandamano ya mara kwa mara.

Mpasuko mkubwa umejitokeza pia ndani ya Baraza la Mawaziri la Netanyahu kati ya baadhi ya mawaziri na vilevile kati ya mawaziri na waziri mkuu mwenyewe.

Baraza la Mawaziri la vita la Israel pia hivi karibuni limeshuhudia mgawanyiko na kuongezeka tofauti na mivutano.

Kanali ya Kiebrania ya Kan imeripoti kwamba Benny Gantz na Gadi Eisenkot, wajumbe wawili wa Baraza la Mawaziri la Vita, wametishia kulivunja Baraza hilo iwapo Netanyahu ataendeleza tabia ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja  kuhusu suala la mateka. Yoav Galant , Waziri wa Vita wa Israel, ambaye naye pia ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Vita, ni miongoni mwa mawaziri wengine wanaopinga uamuzi wa Netanyahu wa kutotuma ujumbe katika mazungumzo ya Cairo.

Kanali hiyo ya Kizayuni imeripoti pia kuwa, mivutano katika baraza la mawaziri la vita la Netanyahu imefikia kiwango cha juu zaidi katika siku za hivi karibuni.

Kwa upatanishi wa Misri, Marekani na Qatar, mazungumzo ya usitishaji vita yalifanyika hivi karibuni mjini Cairo, lakini yalimalizika bila ya kupatikana tija na ikaamuliwa kuwa yataendelea tena katika mji huo.

Pamoja na hayo, Netanyahu ambaye anakazania kuendeleza vita na kumwaga damu za Wapalestina wasio na hatia hayuko tayari kutuma ujumbe kwenye mazungumzo ya Cairo.

Jumatano iliyopita Natenyahu alikataa kutuma ujumbe huko Cairo kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo ya usitishaji vita na kuwekwa wazi hatima ya mateka waliosalia. 

Ofisi ya Netanyahu ilitangaza katika taarifa yake kwamba Israel haitakubali matakwa hewa ya Hamas, na kwamba mazungumzo yataweza kupiga hatua pale tu Hamas itakapobadilisha msimamo wake. Msimamo huo wa Natenyahu umesababisha kuzuka tofauti na mivutano ndani ya baraza lake la mawaziri la vita.

Maandamano Tel Aviv

Gadi Eisenkot, Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la vita, anapinga maamuzi ya upande mmoja yanayochukuliwa na Netanyahu na kuyaelezea kuwa ni ukiukaji wa makubaliano ya baraza hilo. Gazeti la Kizayuni la Maariv pia limeripoti kwamba kwa mujibu wa uchunguzi mmoja wa maoni, kwa akali asilimia 45 ya Waisraeli wanapinga uamuzi wa Netanyahu wa kukataa kutuma timu ya mazungumzo huko Cairo, wakati asilimia 33 tu ndio wanaounga mkono uamuzi huo.

Wakosoaji hao wanaamini kuwa, kwa maamuzi yake hayo ya upande mmoja, Netanyahu anafuatilia zaidi maslahi yake binafsi, ikiwa ni pamoja na kuendelea kubaki madarakani.

Licha ya suala la mazungumzo ya Cairo, hali ya kutoaminiana imezidi kuongezeka kati ya Netanyahu na baadhi ya wajumbe wa baraza lake la mawaziri akiwemo Benny Gantz. 

Kuhusiana na jambo hilo, kanali 11 ya Kiebrania imenukuu chanzo kimoja katika Baraza la Mawaziri la Vita na kufichua kwamba Netanyahu ana wasiwasi kuhusiana na  mazungumzo kati ya Gantz na maafisa wa serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani ambayo yanafanyika moja kwa moja na kupitia njia maalumu. Netanyahu anamchukulia Gantz kuwa mshindani wake katika kuwania kiti cha uwaziri mkuu.

Tags