Mar 08, 2024 07:23 UTC
  • HAMAS: Israel imetibua juhudi zote za kusitisha vita Gaza

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema utawala haramu wa Israel umevuruga jitihada zote za wapatanishi za kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.

Hayo yalisemwa jana Alkhamisi na Msemaji wa HAMAS, Sami Abu Zuhri na kueleza kuwa, utawala wa Kizayuni umekataa kata kata kusitisha vita kikamilifu na kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingizwa katika Ukanda wa Gaza.

Afisa mwingine wa ngazi ya juu wa HAMAS, Mahmoud Mardawi amesema hatima ya mazungumzo hayo sasa yako mikononi mwa Marekani, mshirika mkuu wa utawala wa Kiziayuni.

Mardawi amesema: Marekani sasa ina jukumu la kumshinikiza (Benjamin) Netanyahu na utawala wake (haramu) ufikie makubaliano ya usitishaji vita. Iwapo Israel ipo jadi na haitofanya ajizi, kuna uwezekano wa kufikia makubaliano kabla ya kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kadhalika afisa mwingine wa muqawama wa Palestina aliyeshiriki mazungumzo ya usitishaji vita katika mji mkuu wa Misri, Cairo amebainisha kuwa, "Tunasubiri jibu rasmi la mwisho kutoka kwa adui (Israel)."

Jinai za kutisha za Israel katika Ukanda wa Gaza

Baada ya kupita siku zaidi ya 150, utawala wa Kizayuni wa Israel haujaweza kufikia malengo uliyotangaza kuwa sababu ya kuanzisha vita dhidi ya Ukanda wa Gaza, licha ya kuua maelfu ya Wapalestina, kujeruhi maelfu ya wengine, mbali na mamia ya maelfu walioachwa bila makazi pamoja na kuugeuza ukanda huo kuwa eneo la magofu.

Jihad Taha, Msemaji wa HAMAS amesema ujumbe wa harakati hiyo umeondoka Cairo bila tija yoyote kwenye mazungumzo, na kwamba Israel imekataa kutoa dhamana ya usitishaji vita. Amesema Tel Aviv inakataa kuondoka Gaza na inakataa kuwaruhusu Wapalestina waliolazimika kukimbia makazi yao kurejea makwao.

Tags