Apr 20, 2024 11:10 UTC
  • Wapalestina wengine 37 wauawa shahidi kutokana na Israel kuendeleza mashambulizi Ghaza

Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, Wapalestina wengine 37 wameuawa shahidi na 68 wajeruhiwa katika muda wa saa 24 zilizopita, wakati jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilipoendeleza mashambulizi yake kwenye Ukanda wa Ghaza uliozingirwa.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema: "majeshi ya Israel yamefanya mauaji manne ya familia kadhaa katika Ukanda wa Ghaza, na kuwaua shahidi watu 37 na kuwajeruhi 68 katika muda wa saa 24 zilizopita.
 
Taarifa hiyo imeongeza kuwa watu wengi bado wamenasa chini ya vifusi na barabarani kwa sababu waokoaji hawawezi kuwafikia.
 
Huku ukipuuza uamuzi wa muda wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, utawala wa Kizayuni unaendeleza mashambulizi yake kwenye Ukanda wa Ghaza ambapo Wapalestina wasiopungua 34,049 wameshauawa shahidi hadi sasa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na 76,901 kujeruhiwa tangu Oktoba 7.
Unyama unaofanywa na utawala wa Kizayuni Ghaza unawalenga zaidi wanawake na watoto

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, vita vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Ghaza vimesababisha asilimia 85 ya wakazi wa eneo hilo kuwa wakimbizi wa ndani huku kukiwa na uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na dawa, mbali na asilimia 60 ya miundombinu ya eneo hilo kuharibiwa au kubomolewa kikamilifu.

 
Israel inashutumiwa kwa mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ. Uamuzi wa muda uliotolewa na mahakama hiyo mwezi Januari uliiamuru Tel Aviv isitishe vitendo vya mauaji ya kimbari na kuchukua hatua za kuhakikisha misaada wa kibinadamu inafikishwa kwa raia huko Ghaza.
 
Hata hivyo utawala wa Kizayuni hadi sasa umekaidi kutekeleza agizo hilo.../